NEWS

Monday, 9 March 2026

Tunaipongeza Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara kwa kumulika barabara Hifadhi ya Serengeti



Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara kilichofanyika mjini Musoma hivi karibuni na kukataa kupitisha bajeti ya barabara ya Hifadhi ya Taifa Serengeti

Na Mwandishi Wetu
----------------------------

UamuzI wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara kukataa kupitisha bajeti ya matengenezo ya barabara za Hifadhi ya Taifa Serengeti (SENAPA) kwa mwaka wa fedha 2026/2027 unastahili pongezi za dhati.

Ni uamuzi wa kiuwajibikaji, weledi na uelewa mpana wa umuhimu wa miundombinu ya barabara za hifadhi hiyo ambayo ni moja ya hazina kubwa zaidi za uhifadhi na utalii duniani.

Hifadhi ya Taifa Serengeti siyo tu fahari ya Tanzania, bali ni urithi wa dunia. Kupitia umaarufu wake wa kipekee, hifadhi hii imeendelea kuvutia mamilioni ya watalii kutoka mataifa mbalimbali na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa mapato ya taifa kupitia sekta ya utalii.

Kutokana na umuhimu huo, miundombinu ya hifadhi hiyo, hususan barabara haipaswi kuangaliwa kwa mtazamo wa kawaida - kiasi cha kutengewa bajeti finyu isiyolingana na mahitaji halisi.

Ndiyo maana hatua ya Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara ya kukataa kupitisha bajeti ya shilingi bilioni 3.1 kwa ajili ya matengenezo ya barabara za hifadhi hiyo inastahili kuungwa mkono na wapenda maendeleo wa sekta ya utalii.

Kwa uhalisia wa mahitaji yaliyopo katika hifadhi hiyo kongwe na maarufu duniani - kiasi hicho hakiwezi kukidhi gharama ya matengenezo na maboresho yanayohitajika.

Barabara nyingi ndani ya hifadhi hiyo hukumbwa na uharibifu unaosababishwa na mvua nyingi na hata matumizi makubwa ya magari ya watalii na doria za kuhakikisha usalama wa hifadhi.

Kwa mantiki hiyo, kupitisha bajeti ndogo kungekuwa sawa na kuhalalisha kuendelea kwa matatizo ya miundombinu ya barabara za Hifadhi ya Taifa Serengeti, jambo ambalo lingeathiri kwa kiasi kikubwa utalii, shughuli za uhifadhi na mapato ya taifa.

Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara imeonesha ujasiri wa kiutendaji kwa kukataa kuridhia kiwango cha fedha ambacho hakilingani na ukubwa wa mahitaji ya matengenezo ya barabara za hifadhi hiyo.

Uamuzi huo unastahili kuwa ujumbe kwa wadau wa mipango ya maendeleo kwamba sekta ya utalii inahitaji uwekezaji wa kweli, si wa mazoea. Hifadhi ya Taifa Serengeti ni nembo ya Tanzania katika ramani ya utalii duniani; hivyo miundombinu yake inapaswa kupewa kipaumbele kinachostahili.

Bajeti zinazotengwa lazima ziakisi uhalisia wa mahitaji na thamani ya rasilimali zinazolindwa katika hifadhi hiyo ambayo imekuwa na mwendelezo wa kutunukiwa Tuzo za Hifadhi Bora Afrika.

Uamuzi wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara kukataa kuidhinisha bajeti finyu ya matengenezo ya barabara za Hifadhi ya Serengeti umeonesha umuhimu wa taasisi husika zinavyopaswa kusimama imara katika kulinda maslahi ya umma na rasilimali za nchi.

Naam, wakati mwingine maendeleo hayapatikani kwa kukubali kila kilichowasilishwa mezani, bali kwa kuthubutu kusema hapana pale ambapo kiwango kinachopendekezwa hakiendani na mahitaji halisi.

Kwa ukweli usiopingika, shughuli za utalii katika Hifadhi za Taifa ikiwemo Serengeti, zinategemea miundombinu ya barabara bora kama kiungo muhimu cha kuchochea watalii kutembelea vivutio mbalimbali.

Barabara za Hifadhi ya Taifa Serengeti zikiwa mbovu, shughuli za utalii zitadumaa na hivyo kulikosesha taifa fedha za kigeni zinazohitajika kwa maendeleo ya kisekta nchini.

Kwa msingi huo, ni matarajio ya wadau wengi kwamba SENAPA na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) zitalitazama upya suala hilo na kuandaa bajeti inayolingana na uzito wa kazi za matengenezo na ukarabati wa barabara za hifadhi hiyo.

Hatua hiyo siyo tu itaimarisha miundombinu ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, bali pia italinda hadhi ya Tanzania kama kitovu cha utalii barani Afrika.

Itoshe tu kusema kwamba tunaipongeza Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara kwa kukataa kupitisha bajeti finyu ya barabara za hifadhi hiyo. Ni msimamo unaostahili kupongezwa na kuigwa na taasisi nyingine katika kusimamia rasilimali na miradi ya maendeleo ya taifa.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages