
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, akizungumza kwenye Kongamano la Tano la Idhaa za Kiswahili Duniani linaloanza jijini Arusha, jana.
Arusha
----------------
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema serikali imeanza mazungumzo na UNESCO pamoja na Uongozi wa Kampuni Mama inayomiliki Faceebok, Instagram na WhatsApp (META) ili Kiswahili kitambulike rasmi kwenye majukwaa ya kimtandao.
Hatua hiyo inalenga kuwezesha vijana wanaotengeneza maudhui kwa lugha ya Kiswahili kulipwa malipo makubwa kulingana na kazi zao.
Waziri Makonda aliyasema hayo wakati wa Kongamano la Tano la Idhaa za Kiswahili Duniani lililoanza jijini Arusha, jana Machi 24, 2026.
Alibainisha kuwa licha ya maudhui ya Kiswahili, hususan ya Tanzania kuwa mazuri na kupata watazamaji wengi, warushaji maudhui hayo wanalipwa kidogo kutokana na lugha hiyo kutokuwa rasmi kwenye majukwaa ya mitandao hiyo ukilinganisha na lugha ya Kiingereza,
"Leo hii unamkuta mtu wa Tanzania ana followers zaidi ya milioni tatu, aki- post wanaotazama ni wengi ila hapati pesa kupitia Instagram, Facebook, TikTok, hawawalipi kwa sababu Kiswahili bado watu wa META na wenye platform ya mitandao duniani hawajakitambua kama lugha rasmi,” alisema Waziri Makonda.
Kongamano hilo limeandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), likiwakutanisha wadau wa Idhaa za Kiswahili kutoka ndani na nje ya nchi linalofanyika kuanzia Machi 24 hadi 27, 2026 katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, akiongozana Waziri Makonda wakati akiwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), linapofanyika Kongamano la Tano la Idhaa za Kiswahili Duniani.
No comments:
Post a Comment