NEWS

Friday, 3 April 2026

Mkurugenzi Mkuu EWURA ‘out’



Dkt. James Andilile Mwainyekule

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametengua uteuzi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dkt. James Andilile Mwainyekule.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, jana Aprili 2, 2026, Dkt. Mwaiyukule atapangiwa majukumu mengine.

Utenguzi huo umekuja siku moja baada ya EWURA kutangaza kupanda kwa bei petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini.

Wakati huo huo, Rais Samia amemteua Prof. Palamagamba John Aaidan Kabudi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu).

Kabla ya uteuzi huo, Prof. Kabudi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Ikulu (Kazi Maalum).

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kwamba Reuben Mhamanilo Kwagilwa amehamishwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Dkt. Festo John Dugange yeye amehamishwa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais kwenda kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI anayeshughulikia Masuala ya Elimu.

Naye Balozi Ali Jabir Mwadini ameteuliwa kuwa Katibu wa Rais, wakati Dkt. Eveline Wilbard Munisi ameteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Samia pia amemteua Angela Kizigha kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wake, Balozi Said Othman Yakub amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages