
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.
Na Mwandishi Wetu
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuunganishwa na mifumo ya malipo ya kikanda, hatua inayorahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha ndani na nje ya nchi pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Akizungumza Aprili 3, 2026 jijini Tangier, nchini Morocco, wakati wa mjadala wa mawaziri katika Kikao cha 58 cha Tume ya Uchumi ya Afrika (ECA), Gavana Tutuba alisema hatua hiyo inaifanya Tanzania kuwa sehemu muhimu ya mtandao wa malipo barani Afrika.
“Tanzania ni sehemu ya mifumo ya malipo ya kikanda, ikiwemo Mfumo wa Malipo wa Afrika Mashariki (EAPS) na Mfumo wa Malipo wa Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC RTGS).
“Kwa sasa benki za biashara nchini zinaendelea kujiunga na Mfumo wa Malipo wa Afrika (PAPSS), unaowezesha miamala ya kifedha kati ya nchi za Afrika kwa haraka na ufanisi,” alisema Gavana Tutuba.
Alieleza kuwa kuimarika kwa mifumo hiyo kutachochea biashara ya mipakani na kuongeza ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika, huku akibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kutumia teknolojia ya fedha kuboresha sekta hiyo.
Aidha, alisema uwepo wa mifumo hiyo ni matokeo ya maendeleo ya teknolojia ya fedha (fintech), akisisitiza kuwa BoT inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana wabunifu kupitia majukwaa mbalimbali ili kuibua suluhisho za kidijitali zitakazoboresha huduma za kifedha nchini.
Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Gavana Tutuba alisema teknolojia ya fedha pamoja na ubunifu wa kidijitali vitaendelea kuwa nguzo muhimu katika kujenga uchumi imara, jumuishi na wenye ushindani.
Kikao hicho kiliwakutanisha mawaziri wa fedha, mipango na maendeleo ya uchumi pamoja na magavana wa benki kuu kutoka nchi mbalimbali za Afrika kujadili mwelekeo wa uchumi wa bara hilo na namna ya kuimarisha mifumo ya kifedha.

No comments:
Post a Comment