
Na Mwandishi Wetu
Tarime
--------------
Tarime
--------------
Viongozi wa vijiji, kata, mila, serikali, dini na asasi za kiraia wameungana kuushukuru na kuupongeza Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa jitihada kubwa unazofanya kuchochea maendeleo ya jamii zinazouzunguka.
Walitoa shukrani na pongezi hizo katika kongamano maalum lililofanyika mjini Tarime, mkoani Mara, Ijumaa iliyopita.
Washiriki walikuwa wenyeviti na watendaji wa vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo, madiwani kutoka kata tano zilizo jirani, wawakilishi wa halmashauri za wilaya na mji, wazee wa mila, viongozi wa dini, asasi za kiraia, Jeshi la Polisi na Wakuu wa Wilaya za Tarime na Rorya.
Wilaya ya Tarime ndipo ulipo mgodi wa North Mara unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Genkuru, Juma Elias Kegoye, akichangia mada katika kongamano hilo.
Mada kuu ya kongamano hilo ilikuwa kujadili fursa na namna wananchi wanavyonufaika na fursa za uwekezaji wa mgodi huo.
“Sasa hivi tunaongea lugha moja na mgodi wa Barrick North Mara, siwezi kuusema vibaya wakati unatupa haki yetu - tunapata maendeleo.
“Tutaendelea kuupatia mgodi huu ushirikiano mkubwa ili uendelee kufanya shughuli zake katika mazingira rafiki,” alisema Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Genkuru, Juma Elias Kegoye.
Akizungumzia maendeleo yaliyowezeshwa na Barrick katika kijiji cha Genkuru, Kegoye alisema wamejenga barabara ikiwemo kwenye maeneo ya milima, hivyo kukifanya kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 5,000 kuwa sehemu bora ya kuishi.
Alisema kijiji hicho kimevunja rekodi ya kupokea shilingi billion 2.7 ambazo ni asilimia moja ya mrahaba kutoka mgodi wa Barrick North Mara kuanzia mwaka 2024.
Alibainisha kuwa fedha hizo zimeelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kijijini, huku miundombinu ya barabra, elimu na afya ikipewa kipaumbele.
Aidha, Kegoye alisema wako mbioni kujenga barabara nyingine yenye urefu wa kilomita saba ambayo itawekewa taa, lakini pia wameweza kununua eneo kubwa kwa ajili ya kujenga soko la kisasa la kijiji.
“Sasa hivi tunazibua barabara - milima inapasuliwa, na hata tunafikiria kuweka taa za barabarani katika kijiji chetu kutokana na mapato ya mgodi. Genkuru ya sasa siyo ile ya zamani na hii ni kwa sababu ya Barrick,” alisema.
Kwa upande mwingine, Kegoye alisema wametumia shilingi milioni 66 kununua mashine ya operesheni ya Kituo cha Afya Genkuru - ambayo inatarajiwa kuanza kutoa huduma siku chache zijazo.
Aliongeza kuwa kijiji cha Genguru chenye vitongoji vinne kinajivunia pia kuwa na shule za msingi tatu zenye miundombinu bora ya kufundishia na kujifunzia.
“Tuna shule tatu za msingi katika kijiji chenye vitongoji vinne, na tumekubaliana kujenga shule ya chekechea ya kisasa kwenye kitongoji kimoja,” alisema na kuhoji: “Tungepataje shule tatu kwenye kijiji kimoja kama si uwekezaji wa mgodi wa Barrick North Mara?”
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dkt. Khalifan Haule, akifungua kongamano hilo kwa niaba ya MKuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi.
Diwani wa Viti Maalum kutoka Kata ya Nyamwaga, Mariam Mkono, alisisitiza kuwa maendeleo ya kisekta yaliyowezeshwa na Barrick yanaonekana wazi, hivyo jamii haina ugomvi na mwekezaji huyo.
Sheikh Mtongori wa Msikiti wa BAKWATA Nyamwaga akichangia mada katika kongam,ano hilo.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Justa Magabe, naye aliutaja mgodi wa Barrick North Mara kama mdau mkubwa wa maendeleo kupitia mabilioni ya shilingi unayotoa kugharimia utekelezaji wa miradi mingi kupitia CSR, mbali na fedha za mrabaha unazopeleka kwenye vijiji vitano.
“Tutakuwa hatuna fadhila kama hatutatambua na kuthamini mambo mengi mazuri ambayo Barrick wametufanyia. Wametugusa kwenye sekta nyingi kama vile afya, elimu, maji na barabara.
Justa akichangia mada katika kongamano hilo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini, Mwita Seri, yeye aliomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwapeleka wachimbaji wadogo wa madini kujifunza mambo mazuri katika mgodi wa Barick North Mara.
“Serikali ipeleke wachimbaji wadogo Barrick North Mara wakajifunze - waone mgodi huo unavyojali haki za wafanyakazi na utunzaji wa mazingira,” alisema Seri huku akikemea utumikishaji watoto katika migodi ya madini ya wachimbaji wadogo.
Mkurugenzi wa Shirika la Sheria na Haki za Binadamu la Tuwakombowe Paralegal (TPO) linalofanya shughuli zake katika wilaya za Tarime na Rorya, Bonny Matto, alikemea watu wachache wanaoichafua Barrick ili kujipatia maslahi yao binafsi.
Mratibu wa kongamano hilo, Deusdedit Bugaywa, akiwasilisha mada.
Mwenyekiti wa Wazee wa Mila wa Koo 12 za Kabila la Wakurya katika Wilaya ya Tarime, Mwikwabe Makabe, alisema wanathamini maendeleo ya jamii yanayowezeshwa na mgodi wa Barrick North Mara.
“Barrick wameleta maendeleo makubwa kwa jamii, tuwape ushirikiano ili watu wetu waendelee kupata maendeleo. Sisi wazee wa mila tutaendelea kuunga mkono mgodi huu. Tunaiomba serikali isifumbie macho watu wanaopotosha ukweli kuhusu mgodi huu,” alisema mzee Mwikwabe.
Askofu wa Kanisa la Yesu Tumaini Kuu, Paul Baru, yeye pia aliipongeza kampuni ya Barrick huku akiifafanisha na mti wenye matunda.
Askofu Baru akichangia mada katika kongamano hilo.
Awali, akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dkt. Khalifan Haule, alisema Barrick pia inalipa kodi nyingi serakilini - zenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa.
Dkt. Haule alidokeza kuwa hata wilaya yake ya Rorya imeonja matunda ya uwekezaji wa Barrick baada ya kufadhili ujenzi wa miundombinu ya elimu, yakiwemo mabweni na vyumba vya maabara katika shule za sekondari.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, alitoa wito kwa washirki wa kongamano hilo kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa mgodi huo ambao pia umeajiri mamia ya Watanzania, wengi wao wakiwa vijana.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akizungumza wakati wa kufunga kongamano hilo. (Picha zote na Mara Online News)









No comments:
Post a Comment