
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba,
Dodoma
------------------
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amewakumbusha watendaji wa serikali jukumu la kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotokelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ya maji, umeme, afya, barabara na elimu inasimamiwa ipasavyo ili iwe na tija kwa Watanzania.
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka jitihada kubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo ni lazima itekelezwe kama ilivyokusudiwa.
Dkt. Mwigulu alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Msanga, Chamwino mkoani Dodoma, baada ya kuweka jiwe la msingi mradi wa maji, akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo.
Alisema jukumu kubwa walilonalo watendaji ni kusimamia ipasavyo miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao na kuhakikisha wananchi wananufaika kama ilivyokusudiwa na Rais Samia.
Waziri Mkuu Mwigulu alisema lengo la serikali ni kuhakikisha Watanzania wote wananufaika na rasilimali za taifa kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Aidha, aliwataka Watanzania kujiepusha na watu wanaotumia kivuli cha imani za dini kufanya siasa za majukwaani, huku wakiwa na lengo ovu la kuwagawa wananchi kwa chuki za kiimani na itikadi za kisiasa.
“Ndugu zangu Watanzani, tuendelee kulinda umoja na amani yetu. Kuna watu sasa wanatafuta namna ya kutumia siasa na dini ili kutugawa, tujihadhari na watu wa namna hiyo,” alisisitiza.
Awali, Waziri Mkuu Mwigulu aliweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Miji 28 wilayani Chamwino, ambapo alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia kwa utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati unaokwenda kumaliza changamoto ya maji katika maeneo hayo.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema Wizara ya Maji itahakikisha mradi huo mkubwa unakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika.
“Kupitia Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka fedha nyingi na tayari vijiji 10,758 vimeshafikiwa na huduma ya maji safi na salama na vimebakia vijiji 1,575,” alisema Waziri Aweso.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Usambazaji wa Maji Mijini kutoka Wizara ya Maji, Mhandisi Charles Mafie, alisema mkataba wa mradi huo unatarajiwa kukamilika Agosti 10, 2026 ukiwa na thamani ya shilingi bilioni 17.2 na umefikia asilimia 70.2 ya utekelezaji.
Mradi huo unatarajiwa kuhudumia wananchi zaidi ya 60,000 katika kata za Msanga, Buigiri, Chamwino na Mtumba na kuongeza upatikanaji wa maji safi kutoka asilimia 91 hadi 100 na kuimarisha uzalishaji wa maji kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
No comments:
Post a Comment