NEWS

Monday, 20 April 2026

Marekebisho Mfumo wa Kidigitali wa Leseni za Utafiti Madini mbioni kukamilika



Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

Na Mwandishi Wetu
---------------------------

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema serikali iko mbioni kukamilisha marekebisho ya Mfumo wa Kidigitali wa Leseni za Utafiti wa Madini utakaosimamia hatua zote za utoaji na usimamizi wa leseni hizo.

Amesema mfumo huo utahusisha utoaji wa leseni, uwasilishaji wa taarifa za kila robo mwaka, utoaji wa hati za makosa na hata kufutwa kwa leseni pale inapobidi bila kuhitaji uingiliaji wa moja kwa moja wa binadamu.

“Baada ya mfumo huu kukamilika, hamtaniona tena natangaza kufuta leseni. Leseni itajiondoa yenyewe kupitia mfumo huu. Mfumo utakuletea taarifa zote muhimu, utakukumbusha muda wa kuwasilisha taarifa, utatoa hati za makosa pale inapobidi na hatimaye utafuta leseni moja kwa moja endapo masharti hayatatekelezwa,” amesisitiza.

Waziri Mavunde aliyasema hayo Aprili 16, 2026, wakati akizungumza katika kipindi cha Morning Trumpet kinachorushwa na runinga ya UTV.

Aliongeza kuwa leseni za utafiti ni msingi muhimu wa kuibua migodi mikubwa na ya kati, na kwamba maeneo yanayoshikiliwa bila kuendelezwa yanaikosesha serikali mapato, ajira na fursa katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini.

Alitoa ufafanuzi huo kufuatia uamuzi wake wa Aprili 15, 2026, wa kuielekeza Tume ya Madini kufuta leseni 40 za utafiti wa madini katika eneo la kilomita za mraba 900 (sawa na ekari 188,163), baada ya wamiliki wake kushindwa kutekeleza masharti ya leseni licha ya kupewa hati za makosa.

Aidha, Waziri Mavunde alisema serikali imejipanga kuimarisha usimamizi wa Sheria ya Madini kwa kuondoa tabia ya mazoea iliyokuwepo kwa muda mrefu, akisisitiza kuwa sekta hiyo inahitaji wawekezaji wenye dhamira ya dhati ya kuendeleza rasilimali za madini kwa manufaa ya taifa.

“Sekta ya Madini kuchangia asilimia 10.1 kwenye pato la taifa si jambo dogo. Tanzania tumepiga hatua kubwa. Fikiria kama tafiti kwenye leseni hizi zingekamilika tungekuwa na migodi mingapi mikubwa na ya kati?” alihoji.

Atoa wito kwa vijana wanaopenda kuingia katika sekta ya madini kujiunga na kuanzisha vikundi rasmi ili waweze kufikiwa na serikali kwa urahisi kupitia programu maalum ya Mining for A Brighter Tomorrow inayolenga kuwezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupata leseni, mitaji na vifaa vya uchimbaji.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages