NEWS

Saturday, 30 May 2026

Mashindano ya 30 UMITASHUMTA Mara yazinduliwa, DC Tarime ataka itengenezwe timu bora itakayobeba mkoa kitaifa



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akipiga mkwaju wa penati wakati wa uzinduzi wa mashindano ya UMITASHUMTA Mkoa wa Mara, jana Mei 29, 2026.

Na Godfrey Marwa
Tarime
-------------

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele, amezindua rasmi Mashindono ya 30 Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) Mkoa wa Mara.

Mashindano hayo yanayoshirikisha halmashauri tisa za mkoa wa Mara, yalizinduliwa jana Mei 29, 2026 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Tarime, ili kupata timu bora kwa kila mchezo itakayowakilisha mkoa kwenye ngazi ya taifa.

Meja Gowele akiongozwa na mmoja wa wanamichezo wa mashindano hayo katika viwanja vya Shule ya Sekondari Tarime.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo, Meja Gowele aliwataka waandaaji kutenda haki ili kupata timu bora itakayowakilisha mkoa vizuri ili kupata ushindi.

Aidha, aliwataka wanamichezo husika kudumisha nidhamu katika kipindi chote cha mashidano hayo kwa kuwa michezo ni afya, ajira na fursa kwa kila mmoja kuonesha kipaji chake.

Meja Gowele akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mashindano hayo. Kulia ni Afisa Michezo Mkoa wa Mara, Mwl. Makondo Makondo.

"Mashindano haya ni kama kitalu cha kuzalisha vipaji. Nitumie hadhara hii kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameruhusu michezo hii ifanyike, niwapongeze makocha ambao wameandaa wanafunzi kuja kuonesha vipaji.

"Siri ya mafanikio ni nidhamu na kujituma, kila mmoja atImize wajibu wake, tuchague bila upendeleo. Tunatengeneza timu kwa ajili ya mkoa, usichague mtu kwa kuwa anatoka halmashauri yako, aliye na kipaji apewe nafasi.

"Michezo hii ni upendo, inaleta umoja na mshikamano, umahiri na uhodari. Walimu wazingatie nidhamu, miongozo imayotolewa na TAMISEMI, kusiwepo na mamluki,” alisema Mkuu wa Wilaya Meja Gowele.

Furaha ya mashabiki na washangiliaji uwanjani.

Naye Afisa Michezo Mkoa wa Mara, Mwl. Makondo Makondo, katika taarifa kwa mgeni rasmi, alisema mashindano hayo yanashirikisha wanamichezo 1,131 nq walimu 79 kutoka halmashauri tiza za mkoa wa Mara.

Mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya taifa yatafanyika mkoani Iringa baadaye mwaka huu, yakiwa na kaulimbiu inayosema "Michezo na Sanaa Shuleni, Daraja la Afya na Ushindani wa Kimataifa".

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages