NEWS

Monday, 4 May 2026

Profesa Muhongo: Kilimo kuwa injini ya uchumi wa Tanzania



Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, akizungumza Bungeni mjini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu
Dodoma
--------------

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, amesema kwa miaka mingi ijayo kilimo kitaendelea kuwa injini ya uchumi wa Tanzania, hivyo mkazo mkubwa lazima uwekwe kwenye maendeleo ya sekta hiyo.

Amesema ili kuimarisha kilimo ambacho ni mhimili wa uchumi wa taifa, lazima sekta hiyo ikue kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Prof. Muhongo aliyasema hayo Bungeni mjini Dodoma wiki iliyopita, wakati akichangia Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Alisema kutokana na ongezeko kubwa la watu, dunia bado haijafanikiwa kuondokana na janga la njaa, jambo linalothibitisha kwamba chakula kinahitajika zaidi ili kulisha ongezeko la idadi ya watu.

Mbunge huyo alieleza kwamba Tanzania imefanikiwa kupunguza mfumuko wa bei za vyakula na kuimarisha usalama wa chakula kwa kuongeza uzalishaji.

Hata hivyo, alisema nguvu kubwa lazima iendelee kuwekwa kwenye kuongeza uzalishaji wa chakula ili nchi iweze kujitegemea.

Alisema soko la chakula duniani bado ni kubwa na kwamba linazidi kupanuka zaidi kutokana na kasi ya ongezeko la watu.

Alitoa mapendekezo kadhaa ya kuboresha sekta ya kilimo, ikiwemo kuongeza utafiti wa mbegu na kupanua kilimo cha unwagiliaji mkubwa na mdogo, kama vile ujenzi wa bwawa kubwa la Bugwema lililoko kwenye jimbo lake la Musoma Vijijini.

Mapendekezo mengine ya Prof. Muhongo ni kuongeza zana za kisasa za kilimo na kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea.

Alidokeza kuwa katika kusukuma ajenda ya umwagiliaji, mradi wa ujenzi wa bwawa la Bugwema wenye thamani ya shilingi bilioni 48 utakabidhiwa kwa mkandarasi Mei 9, 2026.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages