NEWS

Monday, 11 May 2026

Profesa Muhongo asisitiza umuhimu wa elimu ya sayansi kukuza uchumi kuelekea Dira 2050



Mbunge wa JImbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo.

Na Mwandishi Wetu
Dodoma
--------------

Mbunge wa Musoma Vijijini na msomi maarufu nchini, Prof. Sospeter Muhongo, amependekeza taifa liwekeze kwenye masomo ya sayansi ili kukabili changamoto zitokanazo na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na uchumi wa kijiditali kuelekea Dira ya Taifa ya 2050.

Prof. Muhongo amesema katika safari ya Dira ya 2050 lazima kuwe na uchumi unaokua kwa kasi kwa zaidi ya asilimia 10 unaoendeshwa na watu wajuzi kama ilivyo kwa mataifa kama vile Singapore, Japan, Finland, Korea ya Kusini, Canada na Uswisi.

Mbunge huyo wa jimbo la Musoma Vijijini aliyasema hayo wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ya shilingi trilioni 2.398, Bungeni jijini Dodoma, wiki iliyopita.

Alisema lazima taifa litathmini mfumo mpya wa elimu wa Tanzania wa 6-4-2-4 ili uweze kuwa kipimo cha ushindani na mifumo mingine duniani kwa nchi ambazo zimefanya vizuri katika maendeleo ya sekta ya elimu.

Hivyo, alitoa rai kwamba wanafunzi milioni 3.43 walioko shule za sekondari kwa sasa, inabidi asilimia 50 ya idadi hiyo wachukue masomo ya sayansi ili kuwaandaa kwa Tanzania ijayo itakayotawaliwa na maendeleo ya sayansi.

Sambamba na hayo, Prof. Muhongo alipendekeza pia kuwepo kwa kasi ya ujenzi wa maabara kwa shule za sekondari kwa ajili ya masomo ya sayansi.

Alisema maabara hizo hazina budi kusimamiwe na mafundi badala ya kuwategemea walimu.

Mapendekezo mengine aliyoyatoa ni pamoja na maktaba zote za shule kuwa na kompyuta ili kupunguza utegemezi wa vitabu vinavyoagizwa kutoka nje.

Hali kadhalika, Prof. Muhongo alipendekeza kuwepo kwa ongezeko kubwa la walimu wa sayansi na kupunguzwa kwa msongamano wa wanafunzi madarasani ili uwiano wa mwalimu na wanafunzi uwe 1:45 kama ulivyokuwa miaka ya nyuma.

Mapendekezo mengine ya mbunge huyo ni kuanzishwa kwa vyuo vya ufundi kila wilaya, kutengwa fedha kwa ajili ya shughuli za utafiti na serikali kuvisaidia vyama vya kitaaluma.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages