
Mfanyabiashara Mtanzania Nyambari Nyangwine (aliyevaa kofia) na wasaidizi wake katika picha na wawekezaji wa nchini Uturuki, jijini Konya, Ijumaa iliyopita.
----------------------------
Mfanyabiashara Nyambari Nyangwine sasa yupo katika nafasi nzuri ya kushirikiana na wawekezaji wa Uturuki kuanzisha kongani ya viwanda nchini Tazania.
Juzi Jumamosi, Nyangwine alitembelea maeneo mbalimbali katika jiji kubwa la viwanda la Konya nchini Uturuki.
“Nimetembelea viwanda vya kutengeneza sola ya umeme, viatu, matofali, milango, madirisha na viwanda vya mazao ya mifugo,” Nyangwine aliliambia Gazeti la Sauti ya Mara kwa njia ya simu kutoka Uturiki, jana.

Wawekezaji wa nchini Uturuki wakimsikiliza mfanyabiashara Mtanzania Nyambari Nyangwine (aliyevaa kofia) alipokutana nao jijini Konya.
Nyangwine ambaye pia ni mwandishi na mchapishaji maarufu wa vitabu nchini Tanzania, yupo Uturuki kwa ziara ya siku saba tangu wiki iliyopita, ambapo ametembelea miji ya Instambul, Ankara na Konya.
Ijuma iliyopita, mfanyabishara huyo wa Tanzania alihudhuria maonesho makubwa ya mashine za ujenzi katika jiji la Konya kwa mwaliko maalumu kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wafanya Biashara wa Jiji la Konya.
“Lengo la hii ziara ilikuwa kushiriki maonesho ya vifaa vya ujenzi nchini Uturuki kwa mwaliko wa Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa jiji la Konya,” alisema Nyangwine.

Mfanyabiashara Mtanzania Nyambari Nyangwine (aliyevaa kofia) na wasaidizi wake katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Jiji la Konya nchini Uturuki.
Nyangwine alisema moja ya maeneo yaliyomvutia zaidi ni kiwanda cha matofali ya block na kuchoma, na ujenzi wa nyumba za kuhamisha kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
“Utengenezaji wa matofali umenivutia sana na nimenunua mashine tayari kwa kuja kuanza kazi,” alisema Nyangwine.
Jiji la Konya ndio mkoa mkubwa katika nchi ya Uturuki na ambalo linaongoza kwa kuwa na viwanda vingi katika nchi hiyo.
“Konya ndio mji mkubwa wa viwanda hapa Uturuki na katika mazungumzo yetu na wawekezaji ambao tunaenda kushirikiana nao kuanzisha industrial park (kongani ya viwanda) wamesema wapo tayari kuja Tanzania kuanzia Oktoba mwaka huu,” alifafanua Nyangwine.
Alisema pia wafanyabishara hao wa Uturuki wameahidi kuanza kutumia Bandari ya Dar es Salaam kufanya biashara na nchi za DR Congo, Zambia, Rwanda, Burundi na Uganda.
“Wamefurahi sana na wamesema wataanza kutumia Bandari ya Dar es Salaam kufanya biashara katika hizo nchi,” aliongeza Nyangwine.

Mfanyabiashara Mtanzania Nyambari Nyangwine (wa nne kutoka kushoto) katika picha ya pamoja na wawekezaji wa nchini Uturuki alipokutana nao jijini Konya.
Ziara hiyo ya Nyangwine imefungua ukurasa mpya wa majadiliano ya kimkakati kati yake na wawekezaji wa Uturuki, ambapo amesema mazungumzo yao yamelenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, teknolojia, kilimo, ajira na elimu ya kitaalamu.
Nyangwine alitaja baadhi ya mambo muhimu waliyojadiliana kuwa ni kushirikiana kuanzisha kongani ya viwanda nchini Tanzania, hatua ambayo inalenga kushirikiana na wawekezaji hao kutumia fursa ya Bandari ya Dar es Salaam kama lango la biashara kwa nchi jirani.
“Mambo muhimu tuliyoongea ni ushirikiano wa kuanzisha kongani ya viwanda nchini Tanzania ili kutumia fursa ya Bandari ya Dar es Salaam kukamata masoko ya nchi za jirani kama Rwanda, Burundi na Zambia,” alisema Nyangwine.

Nyangwine (aliyevaa kofia) akisalimiana na wawekezaji wa nchini Uturuki alipowasili jijini Konya.
Mbali na hayo, Nyangwine alisema wamejadili suala la Teknolojia ya Habari (IT), ambapo wameonesha dhamira ya kushirikiana katika kuwaendeleza wataalamu wa Kitanzania, hususan wale wanaofanya kazi kwenye kampuni zake.
Katika sekta ya kilimo, alisema wamekubaliana kuangalia fursa za kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kabla ya kuyapeleka katika masoko ya kimataifa, jambo ambalo linaweza kuongeza mapato kwa wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda.

Aidha, masuala ya ajira pia yalikuwa sehemu ya mazungumzo yao, huku Nyangwine akisisitiza umuhimu wa kufungua nafasi zaidi kwa vijana wa Kitanzania kupitia uwekezaji wa pamoja na programu za mafunzo ya kitaalamu.
Kwa upande wa elimu, alisema wamejadili ushirikiano wa kuandaa wataalamu wenye uwezo mkubwa wa kuandika vitabu vya kitaalamu katika nyanja mbalimbali ili kukuza maarifa, tafiti na uzalishaji wa maudhui bora ya elimu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Nyangwine pia alipata fursa ya kutembelea shule za msingi na sekondari katika jiji la Konya, Uturuki.

Mfanyabiashara Mtanzania Nyambari Nyangwine (wa pili kutoka kushoto waliosimama) akiwa na wawekezaji wa nchini Uturuki pamoja na wanafunzi katika moja ya shule alizotembelea jijini Konya, Ijumaa iliyopita.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment