
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
--------------------



Dar es Salaam
--------------------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, jana Mei 28, 2026 alifunga rasmi Mafunzo ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi, Kozi Namba 1 ya Mwaka 2025/2026, katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini, jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo kubwa ya kijeshi ilipambwa na gwaride maalum la wahitimu hao, ambapo Rais Samia alipokea salamu ya heshima na kukagua gwaride hilo kabla ya kuzungumza na viongozi, maafisa wa Jeshi la Polisi na wananchi waliohudhuria.
Katika hotuba yake, Amiri Jeshi Mkuu huyo wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini aliwapongeza wahitimu wote 719 kwa kuhimili mafunzo magumu na ya kisasa, na akasisitiza kuwa taifa linatarajia kuona mabadiliko makubwa katika utendaji wao wa kazi mara watakaporipoti kwenye vituo vyao.

Rais Samia alisema utoaji wa mafunzo kwa Jeshi la Polisi ni moja ya nyenzo zinazoliwezesha kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya kiteknolojia, kiuchumi na kisiasa duniani katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao.
Aidha, Rais aliwasisitiza wahitimu hao kwenda kusimamia haki na sheria kwa kuwa kielelezo chema na kuepuka vitendo vya rushwa na uonevu kwani vinachafua taswira ya Jeshi la Polisi.
Alisema tija ya hatua zinazochukuliwa na serikali kuboresha Jeshi la Polisi itapimwa kwa kuangalia matokeo katika maeneo manne yafuatayo:
Moja, matumizi ya rasilimali za Jeshi la Polisi katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Pili, uzingatiaji miiko ya Jeshi la Polisi katika utendaji kazi. Tatu, imani ya wananchi, sekta binafsi na jumuiya ya kimataifa kwa Jeshi la Polisi. Nne, uwezo wa kutambua viashiria vya uhalifu mapema iwezekanavyo.

Rais Samia akiteta jambo na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camillus Wambura.
Pia, Rais alisisitiza umuhimu wa wananchi kupewa elimu ili washiriki kikamilifu katika kubaini na kutoa taarifa za viashiria vya uvunjifu wa amani kupitia Polisi Jamii.
Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kufanyia kazi mapendekezo ya Tume ya Kuangalia Mifumo ya Jinai ili kuongeza ufanisi, uwazi na matumizi ya teknolojia katika kuzuia na kupambana na uhalifu nchini.
Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), wakuu wa vyombo vyenye dhamana ya ulinzi na usalama, viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, pamoja na ndugu na jamaa wa wahitimu waliofurika kushuhudia ndugu zao wakivishwa vyeo vipya.

No comments:
Post a Comment