
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi.
Mara
-------------
Mkoa wa Mara umepiga hatua kubwa katika kuimarisha usalama na amani, hivyo kuuwezesha kuondoka kwenye orodha ya mikoa inayoongoza kwa matuko ya uhalifu nchini.
Hali hiyo inaufanya mkoa huo wa Kanda ya Ziwa kuwa moja ya mikoa bora ya kuishi na kuwekeza nchini.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, matukio ya uhalifu vikiwemo vitendo vya kukatana panga na ukatili wa kijinsia yanaelekea kubaki historia katika mkoa huo.
“Niseme tu, mkoa wa Mara kwa sasa tuko vizuri. Takwimu za Jeshi la Polisi zinaonesha kwamba mkoa wetu sasa haumo kweye mikoa inayoongoza kwa uhalifu hapa nchini, hata kwenye ile 10 ya mwanzo inayoongoza hatumo, unatutafuta kwa tochi,” RC Mtambi amesema.
Kiongozi huyo wa mkoa aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa harambee ya ujenzi wa ofisi za makao makuu ya Kanisa la Waadvenstista Wasabato (SDA) Jimbo jipya la North Mara Filed, wilayani Tarime.
Alisema mageuzi makubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanashuhudiwa katika mkoa huo wenye utajiri mkubwa wa madini na rasilimali nyingine zinatoa fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
“Tunataka Mara ambayo kila mmoja wetu anatazama maendeleo na uchumi, siyo mambo ya mapanga, hongereni sana wana-Mara,” RC Mtambi aliwapongeza wakazi wa mkoa huo kwa hatua hiyo ya kimaendeleo.
Alitumia nafasi hiyo pia kuwashukuru viongozi wa Kanisa la SDA kwa kuendelea kuwa wadau muhimu wa amani katika mkoa wa Mara
“Muendelee kutuongoza katika kuhakikisha kuwa jamii yetu inakuwa na maadili sitahiki,” alisema kiongozi huyo mbele ya mamia ya waumini wa Kanisa la SDA Jimbo la North Mara Field na wageni waliohudhuria changizo hilo.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, alimwakilisha Waziri Mkuu, Dkt Mwigulu Nchemba, kuongoza changizo hilo ambapo kiasi cha shilingi milioni 641 zilipatikana kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za jengo la ofisi za jimbo jipya la North Mara Field.
Jengo hilo la ghorofa mbili litajengwa katika eneo la Kibumaye, nje ya kidogo ya mji wa Tarime.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment