
Mkurugenzi wa Kemanyanki Contractors, Manpower & General Supplies, Nicholaus Mgaya “Chichake” (wa pili kushoto mbele) na baadhi ya wafanyakazi wake katika picha ya pamoja.
Tarime
------------
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unatekeleza Sera ya ‘Local Content’ kwa vitendo kwa kuwashirikisha wazawa kwenye mnyororo wa sekta ya madini, wengi wao wakiwa ni ambao wanatoka maeneo yanayozunguka mgodi huo unaoendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.
Sera hiyo inazitaka kampuni za uchimbaji madini kuwajengea uwezo na kuwapa Watanzania fursa za biashara na ajira ili kukuza uchumi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ndogo ya The Mining (Local Content) Regulations ya Mwaka 2018.
Miongoni mwa kampuni za wazawa zinazonufaika na fursa za zabuni za huduma mbalimbali za kibiashara katika mgodi huo wa Barrick North Mara ni Kemanyanki Contractors, Manpower & General Supplies.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Nicolaus Mgaya maarufu kwa jina la Chichake, ni mmoja wa wakandarasi wazawa wanaojivunia uwepo wa mgodi huo na milango ya fursa za kiuchumi zilizopo.
“Mazingira kwa sasa katika mgodi wa Barrick North Mara ni mazuri na fursa ni nyingi, kinachohitajika kwa sasa ni wananchi wanaoishi jirani na mgodi kuchangamkia fursa zilizopo na kuuona kama mali yao.
“Mgodi kwa sasa ni wa kwetu na ni sehemu ya jamii - sio wa kuvamia,” Chichake alisisitiza wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mfuko wa Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara, iliyofanyika hivi karibuni kwenye Hoteli ya CMG, mjini Tarime.
Hafla ya uzinduzi huo ambayo ilifanyika sambamba na maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Mkoa wa Mara, ilihudhuriwa na waandishi wa habari kutoka wilaya zote za mkoa huo, viongozi wa serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Mkurugenzi Chichake akifurahia jambo huku akiendelea na kazi ofisini kwake
Kemanyanki ilivyopata nguvu ya kuajiri vijana
Kwa mujibu wa Chichake, kampuni yake ya Kemanyanki Contractors, Manpower & General Supplies inapata zabuni nyingi zikiwemo za ujenzi na huduma mbalimbali katika mgodi wa Barrick North Mara.
“Tunafanya kazi na mgodi, zikiwemo za ujenzi (civil and building) na huduma mbalimbali,” alisema Chichake na kubainisha kuwa kampuni yake imeajiri watu zaidi ya 170 kwa kazi za kudumu na muda mfupi, wengi wao wakiwa vijana kutoka vijiji vinavyozunguka mgodi huo.
Aidha, alisema wafanyakazi zaidi ya 600 wamenufaika na ajira katika kampuni yake kati ya mwaka 2023 na 2026, ambapo asilimia 90 ya ajira hizo ziligusa wakazi wa vijiji vilivyo jirani na mgodi.
“Asilimia 70 ya wafanyakazi wetu waliokuwa na hali duni - sasa hivi wamejenga makazi ya kudumu,” alisema Mkurugenzi Chichake.
Mbali na ajira, Kemanyanki imekuwa ikisaidia jamii kwa kuchangia vifaa vya shule na michezo, kusaidia ada na michango ya shule kwa baadhi ya wafanyakazi wake na kufadhili walimu wa masomo ya sayansi katika shule zenye upungufu wa walimu hao.
Mkurugenzi Chichake (wa pili kulia) akiwa na baadhi ya wafanyakazi wake katika moja ya maeneo ya miradi wanayotekeleza.
Chichake aliweka wazi kuwa ushirikiano unaotolewa na mgodi wa Barrick North Mara ndio umekuwa chachu ya mafanikio ya kampuni hiyo na maendeleo ya jamii inayouzunguka.
“Tunaishukuru sana kampuni ya Barrick kwa kutengeneza fursa endelevu za kunufaisha jamii inayozunguka mgodi wa North Mara,” alisema Chichake.
Alisema ajira zinazotolewa na kampuni yake ya Kemanyanki Group zimesaidia pia kupunguza wimbi la vijana ambao walikuwa wakivamia mgodi huo kwa lengo la kuiba mawe ya dhahabu.
Takwimu kutoka serikalini zinaonesha kuwa kwa sasa vitendo vya uvamizi katika mgodi huo vimeshuka kwa asilimia 99, huku mahusiano ya mgodi na jamii yakiwa yameimarika zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma.
“Mahusiano ya mgodi wa North Mara kwa sasa ni mazuri na hata matukio ya uvamizi mgodini yamepungua hadi wastani wa mtu mmoja kwa siku,” Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, aliwambia waandishi wa habari ofisini kwake, hivi karibuni.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele.
Uwekezaji mkubwa kwenye mgodi wa North Mara umeshuhudia uwepo wa fursa nyingi za ajira kwa wazawa katika kampuni ya Barrick, lakini pia kwa wakandarasi wazawa wanaopata fursa za kibiashara mgodini hapo.
Taarifa zilizopo zinaonesha kwamba hadi sasa mgodi wa Barrick North Mara umesajili kampuni zaidi ya 100, nyingi zikiwa za wazawa - ambazo zinapata fursa mbalimbali za kibiashara katika mgodi huo.
“Ajira kwa wazawa zimekuwa nyingi sio tu kutoka Barrick bali pia kutoka kwa wakandarasi wa mgodi ambao wengi wao pia ni wazawa na wanatoa ajira nyingi kwa vijana,” alisema Meja Gowele.
Aidha, mauzo ya kampuni za wazawa katika mgodi huo yanaripotiwa kuongezaka mwaka hadi mwaka.
Hivyo, Chichake aliwaomba waandishi wa habari kutangaza mageuzi makubwa ya maendeleo na mambo mazuri yanayofanyika katika maeneo yanayozunguka mgodi huo, ukiwemo mji mdogo wa Nyamongo.
“Kuna maendeleo makubwa ya kuripoti kwenye vyombo vya habari kuhusu maeneo yaliyo jirani na mgodi huu wa North Mara, tembelea mjionee,” alisema Chichake ambaye ni mzaliwa wa Nyamongo.
Mgodi huo ambao umeajiri mamia ya watu huku asilimia kubwa wakiwa Watanzania, umeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara na taifa kwa ujumla.
Barrick inatekeleza Sera ya ‘Local Content’ kwa vitendo kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo yanayozunguka shughuli zake za uchimbaji madini.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

.jpg)
No comments:
Post a Comment