NEWS

Friday, 26 June 2026

Mtambi ahimiza mshikamano wa madiwani Manispaa ya Musoma



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma jana.

Na Godfrey Marwa
Musoma
----------------

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amewataka madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma kuzika tofauti zao ili kutekeleza majukumu yao ya kikatiba katika kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Kanali Mtambi alitoa maelekezo hayo mjini Musoma jana katika kikao maalum cha baraza la madiwani hao kilichojadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2024/2025.

Sehemu ya madiwani hao kikaoni. (Picha zote na Mara Online news)

"Niwasihi mhakikishe mnatendea haki imani ya wananchi ili matarajio yao ya kimaendeleo yatimie, mkishindwa baraza litakuwa limepoteza sifa, tujikite kutimiza majukumu yetu ya kisheria,” alisema Kanali Mtambi baada kubaini uwepo wa mgawanyiko miongoni mwa madiwani hao.

Aliongeza: "Kuna mambo tunayapuuza, sio kwamba hatusikii, tunayaona na tutayafuatilia, serikali haiachi jambo ambalo haliko sawa liendelee, niwasihi tekelezeni wajibu wenu. Ni matarajio yangu mwaka huu tunaomalizia tutapata hati safi na kwenye nidhamu iwe hati safi.”

Kwa upande wake Meya wa Manispaa hiyo, Alex Mtaki Nyabiti, aliahidi kuyafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa, huku akiomba ushirikiano kwa watumishi waliosababisha uzembe na dosari za halmashauri hiyo kwenye hoja kwa CAG.

"Yeyote aliyeguswa kwenye kitabu hiki aende akatoe ushirikiano kwa mamlaka ili kuyamaliza kwa maslahi ya Manispaa na wananchi,” alisema Meya Nyabiti.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages