
IGP Camillus Wambura (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa nyumba tatu pacha za makazi ya askari polisi wa Tarime Rorya. Wengine ni RPC wa Tarime Rorya, SACP Mark Njera (wa pili kulia), Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dkt. Khalifan Haule (wa pili kushoto), RPC Mkoa wa Mara, SACP Pius Lutumo (kulia) na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl. Saul Mwaisenye.
NA MWANDISHI WETU,
Tarime
------------------------------------------------
MKUU wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camillus Wambura, amempongeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime Rorya, SACP Mark Njera, kwa kubuni na kuanzisha mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya askari wa jeshi hilo katika mkoa huo.
“Leo ni siku ya faraja kwangu kwa kuona watu wanapojiletea maendeleo badala ya kusubiri, nakupongeza sana kwa ubunifu huu,” IGP Wambura alitoa pongezi hizo kwa SACP Njera katika sehemu ya hotuba yake wakati wa uzinduzi wa mradi huo wilayani Tarime, Ijumaa iliyopita.
Pia, alizundua nyumba tatu zenye uwezo wa kuhudumia familia sita katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na maafisa wa Jeshi la Polisi, viongozi wa serikali na wadau kutoka taasisi za umma na binfasi katika mkoa huo.
Nyumba hizo zimejengwa kwa thamani ya shilingi zaidi ya milioni 300.
“Leo polisi Tarime Rorya, mmetupatia somo kubwa, ninyi mmetuonesha jambo tofauti. Naona heshima na matumani kwa askari wetu,” alisema IGP Wambura.
Alisema ubunifu huo unapaswa kuigwa na mikoa mingine nchini.
“Huu sio uwekezaji kwa askari, bali ni uwekezaji kwa usalama wa wananchi na taifa zima. Hili ni somo kubwa kwa Jeshi la Polisi. Hongereni Tarime Rorya, mmeonesha njia,” alisema.
Aidha, IGP huyo alikubali ombi la SACP Njera la kuunga mkono mradi wa ujenzi wa nyumba za askari katika maeneo ya Sirari, Nyamwaga na Nyamongo.
“Nimepokea ombi la kupanua mradi huu na naunga mkono. Nipo tayari kuendelea kushirikiana nanyi [Polisi Tarime Rorya] ili kuleta matokeo chanya zaidi,” alisema IGP Wambura.
No comments:
Post a Comment