NEWS

Tuesday, 2 June 2026

Waziri Gwajima: Serikali imeimarisha malezi, ulinzi, ustawi wa watoto nchini



Waziri Dkt. Dorothy Gwajima akiwasilisha Bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni, jijini Dodoma jana.

Na George Shirati
Dodoma
--------------

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema serikali imeendelea kuimarisha malezi, ulinzi na ustawi wa watoto nchini, kupitia programu mbalimbali zinazolenga kujenga kizazi chenye maadili, afya bora na uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa.

Waziri Gwajima aliyasema hayo jana Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha Bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Alisema watoto ni rasilimali muhimu na mtaji wa taifa, hivyo wanapaswa kulelewa katika mazingira salama, yenye upendo na maadili ili kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Aliongeza kuwa serikali inaendelea kutekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (2021/22–2025/26), inayolenga kuongeza kiwango cha ukuaji timilifu wa watoto wenye umri wa miaka chini ya minane kutoka asilimia 47 hadi asilimia 90 ifikapo mwaka 2050.

Aidha, katika kuimarisha malezi ya watoto, Waziri Gwajima alisema wizara hiyo imeanzisha mifumo ya kisasa ya kukusanya na kufuatilia takwimu za malezi na makuzi ya watoto, huku maafisa 227 kutoka ngazi mbalimbali wakipatiwa mafunzo ya usimamizi wa mifumo hiyo.

Waziri huyo alisema serikali pia imeongeza juhudi za kulinda watoto dhidi ya ukatili mtandaoni kufuatia ongezeko la matumizi ya teknolojia, ambapo takwimu zinaonesha asilimia 67 ya watoto wenye umri wa miaka 12 hadi 17 hutumia simu janja.

Alieleza kuwa wawezeshaji 516 walipatiwa mafunzo ya usalama wa watoto mtandaoni na kufanikiwa kuwafikia wanafunzi zaidi ya milioni 1.8, walimu 679 na watumishi wasio walimu 232 katika mikoa yote 26 nchini.

Vilevile, alisema serikali imeanzisha Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu Usalama wa Mtoto Mtandaoni na ipo katika hatua za majadiliano ya kuanzisha matumizi ya Laini Maalum ya Simu kwa Mtoto (Child SimCard) kwa lengo la kuongeza usalama wa watoto katika matumizi ya teknolojia na mawasiliano.

Katika kuimarisha ulinzi wa mtoto shuleni, Waziri Gwajima alisema walimu 4,388 wamepatiwa mafunzo ya kusimamia afua za ulinzi na usalama wa mtoto, huku madawati 3,204 mapya ya ulinzi wa mtoto yakianzishwa na kufanya jumla kufikia madawati 11,156 nchini.

“Serikali pia imeendelea kuwashirikisha watoto katika maamuzi yanayowahusu kupitia Mabaraza ya Watoto, ambapo mabaraza 223 mapya yameanzishwa na kufanya jumla kufikia 8,427 kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa, alisema Waziri Gwajima.

Kuhusu vita dhidi ya ukeketaji, alisema serikali imezindua Mkakati wa Taifa wa Kisekta wa Kutokomeza Ukeketaji wa mwaka 2025/26 hadi 2029/30, unaolenga kupunguza kiwango cha ukeketaji kutoka asilimia nane hadi asilimia nne ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wa watoto walio katika mazingira hatarishi, Waziri Gwajima alisema watoto zaidi ya 284,000 wametambuliwa na kupatiwa huduma mbalimbali za kiustawi ikiwemo elimu, afya, mafunzo ya ufundi stadi na kuunganishwa na familia zao.

Aidha, watoto 6,182 waliokuwa wanaishi na kufanya kazi mitaani wameokolewa kupitia kampeni maalum ya kitaifa, huku serikali ikianzisha madawati 14 ya huduma za ustawi wa jamii katika vituo vikuu vya usafiri nchini yaliyosaidia kuokoa watoto 3,366 na kuwaunganisha na familia zao.

Katika kulinda haki za watoto kupitia mfumo wa sheria, alisema mashauri 1,367 yalisikilizwa katika Mahakama za Watoto kati ya Julai 2025 na Aprili 2026, huku watoto 154 waliokinzana na sheria wakipatiwa huduma za marekebisho ya tabia na stadi za maisha katika vituo maalum.

Pia, Waziri Gwajima alisema serikali imeendelea kuimarisha huduma za malezi ya awali kwa kusajili vituo 922 vya kulelea watoto mchana, na kufanya jumla ya vituo hivyo kufikia 4,916 vinavyohudumia watoto zaidi ya 565,000 nchini.

Pamoja na mafanikio hayo, alisema changamoto ya ukatili dhidi ya watoto bado ipo, ingawa takwimu zinaonesha idadi ya watoto walioripotiwa kufanyiwa ukatili wa kingono imepungua kutoka 10,937 mwaka 2024 hadi 9,902 mwaka 2025.

Alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya ukatili wa watoto si jukumu la serikali pekee, bali ni wajibu wa jamii nzima, wakiwemo wazazi, walezi, viongozi wa dini, walimu na wananchi kwa ujumla kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama, yenye maadili na heshima kwa utu wa binadamu.

Waziri Gwajima alibainishwa kuwa wazazi na walezi 469,634 wamepatiwa elimu ya malezi chanya kupitia majukwaa mbalimbali nchini, huku vikundi 4,526 vya malezi na matunzo ya watoto vikianzishwa chini ya kaulimbiu ya "Familia Bora, Taifa Imara."

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages