
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya, SACP Mark Njera (wanne kushoto mbele) katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati mpya ya Usalama Barabarani ya mkoa huo mara baada ya kuizindua Jumatatu Julai 20, 2026.
Tarime
------------
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya, SACP Mark Njera, amezindua Kamati mpya ya Usalama Barabrani ya mkoa huo na kuielekeza kuleta matokeo chanya ya kupunguza ajali za barabarani.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa ofisi zake Jumatatu Julai 20, 2026, RPC Njera alisema pamoja na mambo mengine, kamati hiyo ina jukumu la kufanya utafiti wa kujua vyanzo vya ajali na viashiria, kisha kushauri au kuweka mipango madhubuti itakayosaidia kupunguza ajali za barabarani.
Alisema ajali za barabarani zinapotesha nguvu kazi ya taifa na kuingiza familia husika katika huzuni na hali ngumu ya maisha.

“Kwa mujibu wa sharia, Kamati ya Usalama Barabarani ni chombo kikubwa cha kusimamia masuala ya usalama barabarani. Fanyeni tafiti kubaini vyanzo vya ajali na kutafuta suluhu,” Kamanda Njera alisema katika sehemu ya hotuba yake wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo.
Alitaka kamati hiyo pia kutoa elimu ya masuala ya usalama barabarani kwa watumiaji wa barabara, wakiwemo waendesha pikipiki (bodaboda) katika maeneo yote ya wilaya za Tarime na Rorya zinazounda mkoa huo wa kipolisi.

“Ninavyoona wajumbe wa kamati hii wote ni potential (mnaweza kufanya vizuri). Nina imani mtafanya vizuri na matarajio yangu ni kuona ajali za barabarani zinapungua katika mkoa wa kipolisi wa Tarime Rorya,” alisema RPC Njera.
Viongozi wapya wa kamati hiyo na ni Mkurugenzi wa Kampuni ya RIN, Isack Charles Range (Mwenyekiti), Mkurugenzi wa Soya One Limited, Chacha Marwa Gesora (Makamu Mwenyekiti) na Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya, Ibrahimu Wembo (Katibu).

(Picha zote na Mara Online News)
Wajumbe wa kamati hiyo ni Meneja wa TRA Wilaya ya Tarime, Kenedy Sawaya, Meneja wa TARURA Wilya ya Tarime, Mhandisi Charles Marwa, Mwakilishi kutoka sekta ya afya, Joshua Makoa, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote na Mkurugenzi wa Professor Mwera Foundation (PMF), Hezbon Peter Mwera.
Wengine ni Mwenyeketi wa Madereva wa Magari ya Abiria, Joseph Magori na mwanahabri Jacob Mugini ambaye ni Mkurugeni wa Mara Online na Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Sauti ya Mara, Remmy Bathoromea Machage, Ongujo Wakibara, Joseph Cornelius na Ayoub Ally Rajab.
Kamati hiyo itafanya kazi kwa muda wa miaka mitatu, kwa mujbu wa sheria.
No comments:
Post a Comment