
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Madini jijini Dar es Salaam jana.
Dar es Salaam
---------------------
Shilingi trilioni 5.5 zimetumika katika ununuzi wa huduma na bidhaa mbalimbali ndani ya migodi nchini Tanzania, hatua inayodhihirisha mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Sera ya Ushirikishwaji wa Wazawa (Local Content) kwenye sekta ya madini.
Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, wakati akifungua Kongamano la Madini katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba.
Dkt. Kiruswa alisema fedha hizo ambazo hapo awali zilikuwa zikienda kwa kampuni za nje ya nchi, sasa zimebaki mikononi mwa wafanyabiashara, wakandarasi na watoa huduma wa Kitanzania.
Takwimu za ununuzi migodini zinaonesha kuwa kiasi hicho cha fedha kimeelekezwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo uhandisi na ujenzi, ukandarasi wa ujenzi wa miundombinu ya migodi na barabara, nishati na mafuta pamoja na usambazaji wa nishati ya mafuta ya dizeli kwa ajili ya kuendesha mitambo.
Naibu Waziri Kiruswa alitaja sekta nyingine kuwa ni huduma za jamii, utoaji wa chakula, ulinzi, usafirishaji wa wafanyakazi na vifaa vya kinga kazini (PPE).
Alitoa wito kwa sekta binafsi na taasisi za kifedha kuendelea kuwajengea uwezo wa kifedha na kiufundi wajasiriamali wazawa ili waweze kushindana katika zabuni kubwa zaidi, hususan za ununuzi wa mitambo mizito na vipuri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwase, alisema shirika hilo inaunga mkono juhudi za serikali katika ajenda ya nishati safi ya kupikia kwa kuandaa mradi wa Rafiki Briqutte.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati, aliipongeza serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kukuza uchumi wa taifa kupitia uongezaji thamani madini pamoja na kutoa ajira kwa vijana kupitia mnyororo wa thamani wa madini.


No comments:
Post a Comment