
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akipokea gawio la shilingi bilioni 221.9 kutoka kwa Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido (kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya Twiga Minerals, Mathias Chanila, Ikulu jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
--------------------------
Katika kipindi cha miaka takriban saba iliyopita tangu Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga kuingia ubia na kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick, yamepatikana mafanikio makubwa yanayodhihirisha umuhimu wa ushirikiano wa serikali na sekta binafsi.
Mafanikio haya yanaenda sambamba na mchango wa taifa kwenye sekta ya madini katika Pato la Taifa ambao kwa sasa unachangia asilimia 10, ambapo Barrick na Twiga kupitia uendeshaji wa migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi ulio kwenye mchakato wa kufungwa inachangia kwa kasi kubwa ukuaji wa sekta hiyo.
Tangu ubia wa Barrick na Twiga uanze tumeshuhudia ukichangia kulipa kiasi kikubwa cha kodi serikalini na kuongoza katika kutoa gawio, mrabaha na kufanikisha utekelezaji miradi ya kijamii katika sekta za afya, elimu, maji safi, miundombinu ya barabara, ajira kupitia fedha za Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) na kunufaisha wazabuni na wakandarasi wa ndani.
Katika kipindi cha mwaka huu, Barrick-Twiga imeweka rekodi ya mafanikio kwa kutoa gawio kubwa serikalini kati ya kampuni zaidi ya 300 ambazo serikali ina hisa, ambapo imetoa shilingi bilioni 221.9, ikiwa ni mwendelezo wa kutoa gawio serikalini.
Katika miaka iliyopita - mwaka wa fedha 2021/2022 ilitoa shilingi bilioni 53.5, 2022/2023 (bilioni 84) na 2024/2025 (bilioni 93.6).
Mbali na kutoa gawio nono, Barrick-Twiga hivi karibuni ilitangazwa na kutunukiwa Tuzo ya Rais ya Mlipa Kodi Bora katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2024/2025 wakati wa hafla ya siku ya kuwatambua walipa kodi bora nchini iliyoambatana na maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mafanikio haya ya kuwa kinara wa kutoa gawio na kodi mwaka huu, yamekuja wakati kampuni ya Barrick hivi karibuni ilitoa ripoti ya utekelezaji wa masuala endelevu mwaka uliopita, ikibainisha kwa kina utendaji wa shughuli zake katika sehemu mbalimbali duniani na kuweka msisitizo wa kuendelea kufanya uwekezaji wenye kuleta manufaa kwenye maeneo ya biashara zake.
Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Hill, akizungumzia ripoti hiyo, alisisitiza kuwa kampuni itaendelea kutekeleza sera zake madhubuti ambazo zinaendelea kuleta mafanikio.
"Tunapoingia katika awamu mpya ya kusisimua ya ukuaji na kupata mafanikio, uendelevu unasalia kuwa msingi wa jinsi tunavyofanya kazi,” alisema Hill na kuongeza:
“Kanuni ambazo zimetuongoza kwa miaka mingi bado hazijabadilika: kuwaweka watu wetu salama, uchimbaji madini kwa uwajibikaji, kujenga ushirikiano imara na kutoa thamani ya muda mrefu ambayo inashikiriwa na washikadau wetu wote.”
Ripoti hiyo imebainisha kuwa hadi mwaka jana, asilimia 96 ya wafanyakazi wa Barrick sehemu mbalimbali duniani, ikiwemo Tanzania na asilimia 76 ya wazabuni wake walitoka katika nchi mwenyeji, ambapo pia kampuni ilitumia Dola za Marekani bilioni 7.1 katika matumizi na wasambazaji wa ndani, huku nchi mwenyeji pia ikiwekeza dola milioni 62 katika mipango ya maendeleo ya jamii.
Kwa hapa Tanzania, uekelezaji wa mkakati huu endelevu unaendelea kufanikisha masuala mbalimbali, ambapo tangu ubia wa Barrick na Twiga uanze mwaka 2019, Barrick imewekeza dola bilioni USD 4.79 katika uchumi wa Tanzania kupitia kulipa kodi na tozo mbalimbali, gawio, mrabaha, mishahara, malipo ya wazabuni wa ndani na utekelezaji wa miradi ya kijamii.
Barrick imekuwa ikitekeleza Sera ya Maudhui ya Ndani (Local Content) kwa vitendo, ambapo inafanya manunuzi ya bidhaa za uzalishaji kwa asilimia zaidi ya 90 kutoka kwa wazabuni wa ndani na asilimia 96 ya wafanyakazi wake ni Watanzania, wakiwemo wanaotoka maeneo ilipo migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu. Pia, viongozi wote wa nafasi za juu katika uendeshaji wa shughuli zake hapa nchini ni Watanzania.
Baadhi ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Barrick-Twiga ambayo itaacha alama kwa vijazi vizavyo ni mradi wa kusongesha mustakabali wa elimu nchini- ‘Barrick-Twiga Future Forward Education Program’ ambao umelenga kuongeza na kuboresha miundombinu ya shule za elimu (advanced level) ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaochaguliwa waliokuwa wanakosa fursa ya kuendelea na masomo kutokana na uchache wa miundombinu na kuhakikisha wanapata elimu katika mazingira rafiki.
Mradi huu ambao umeingia katika awamu ya pili utagharimu shilingi zaidi ya bilioni 70.5 ukilenga kujenga vyumba vya madarasa 1,090, majengo ya maliwato na vyoo 1,660 pamoja na mabweni 270 katika shule 161 nchini kote.
Katika awamu ya kwanza imefanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa vya kisasa 374, mabweni ya kisasa 89 na vyoo 569.
Wakati mradi umeingia awamu ya pili, mafanikio yake yameanza kuonekana kupitia matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) hivi karibuni, ambayo imeonesha kuwa watahiniwa 124,603 sawa na asilimia 99.56 wamepata ufaulu mzuri wa daraja la kwanza hadi la tatu na kuendeleza rekodi ya mwaka uliotangulia, ambapo wanafunzi walisoma katika mazingira mazuri ya miundombinu iliyoboreshwa.
Pia, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imebainisha kuwa nafasi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu nchini kwa masomo ya shahada ya kwanza zimeongezeka kufikia 170,000.
Mradi mwingine wa Barrick utakaoacha alama ni wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Kahama-Bulyanhulu JCT- Kakola yenye urefu wa kilomita 73 unaotekelezwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation kwa ufadhili wa migodi ya Barrick-Twiga kwa gharama ya shilingi bilioni 101.2 ambao ujenzi wake unaendelea.
Mbali na kuwekeza katika miundombinu, Barrick-Twiga pia imejikita kujenga kizazi cha wataalamu wa baadaye wa sekta ya madini, ambapo hivi karibuni ilisaini mkataba wa miaka 10 na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ili kutoa shilingi bilioni 25 kwa ajili ya ufadhili wa masomo kwa wanafunzi zaidi ya 500, kuwezesha tafiti na kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa madini na jiolojia kupitia ‘UDSM School of Mines and Geosciences (SOMG)’.
Pia, Barrick-Twiga imetoa ufadhili kwa wanafunzi watano Watanzania kupata utaalamu wa fani ya madini nchini Afrika ya Kusini.
Mafanikio mengi yaliyopatikana kupitia ubia huu yanadhihirisha kuwa serikali ikifanya kazi kwa ushirikiano na sekta binafsi taifa letu litaweza kupata maendeleo ya haraka.
Kama kampuni moja imeweza kuleta mafanikio haya inadhihirisha kwamba tukiwa na kampuni kubwa nyingi zinazoendeshwa kwa weledi kama Barrick katika sekta mbalimbali, taifa letu linaweza kusonga mbele kimaendeleo kwa haraka zaidi.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment