
Wahitimu wa Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Mwera Vision wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wakati wa mahafali yao yaliyofanyika kwenye viwanja vya TVTC mjini Tarime, jana Ijumaa, Agosti 28, 2026.
Tarime
-------------
Mahafali ya Sita ya Wahitimu wa Darasa la Saba na Darasa la Awali katika Shule za Awali na Msingi Mwera Vision yalifanyika jana Ijumaa, Agosti 28, 2026 kwa mafanikio kwenye viwanja vya Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime (TVTC).
Wahitimu wa darasa la saba ni 18 na wa darasa la awali ni 40, ambao hao wa darasa la saba wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Taifa Septemba 9 na 10, mwaka huu.

Wahitimu wa Darasa la Awali katika Shule ya Mwera Vision wakifurahia picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wakati wa mahafali yao jana Ijumaa.
Mkurugenzi wa Professor Mwera Foundation (PMF) inayomiliki shule hizo, Hezbon Peter Mwera, alitumia nafasi hiyo kuendelea kutangaza ofa ya kuwasomesha bure wahitimu hao wa darasa la saba watakaojiunga na Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko ambayo pia inamilikiwa na taasisi hiyo.
"Mwaka jana, vijana waliohitimu hapa tuliwapa ofa ya kusoma Sekondari ya Tarime Mchanganyiko kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne bure. Kwa hiyo na hawa vijana 18 wanaohitimu leo pia tutawasomesha bure katika shule yetu ya Tarime Mchanganyiko," alisema Hezbon.

Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera, akizungumza katika mahafali hayo.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mkurugenzi wa Kampuni ya RIN, Isack Charles Range, aliyewakilishwa na Joseph Mang'era Mahando, alitoa fedha taslimu shilingi milioni 1.5 kusaidia utatuzi wa changamoto zinazoikabili shule hiyo, vikiwemo vyanzo mbadala vya umeme na maji.
"Mgeni rasmi (Mkurugenzi wa RIN) alinituma niwakabidhi pesa milioni moja na laki tano ili zisaidie changamoto mbalimbali zinazowakabili, lakini maombi yenu yote, hasa hili la bweni nitalifikisha kwake na naamini atalishughulikia," alisema Mang'era.

Mang'era (wa pili kulia) akikabidhi shilingi milioni 1.5 kwa Mkurugenzi wa PMF, Hezbon.
Awali, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mwera Vision, Maria Daniel Tarimo, alisema wahitimu hao 18 wa darasa la saba walijiunga na shule hiyo mwaka 2020.

Mwalimu Maria akizungumza katika mahafali hayo
Mahafali hayo pia yaliambatana na ukaribisho rasmi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza "welcome form one" waliojiunga na Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko mwaka huu.

Mwakilishi wa mgeni rasmi akikata utepe shuleni hapo wakati wa sherehe za mahafali hayo

Mkurugenzi wa PMF, Hezbon (kushoto), akikabidhi tuzo kwa mwakilishi wa mgeni rasmi. (Picha zote na Mara Online News)
Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime kinachomilikiwa na PMF kinafundisha fani mbalimbali, zikiwemo za ufundi magari, umeme, mabomba, uhazili, udereva, ushonaji, uongozaji watalii na upishi, miongoni mwa nyingine.
Mbali na chuo hicho cha TVTC, Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko na Shule ya Awali na Msingi Mwera Vision, Taasisi ya PMF inamiliki pia Jogging Club, Mwera Jazz Band na PMF Restaurant.
No comments:
Post a Comment