NEWS

Tuesday, 11 August 2026

Mtumishi matatani kwa kuomba fedha mgonjwa apewe huduma inayotolewa bure




Na Mwandishi Wetu

Mtumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Kwangwa ameingia matatani kwa kuomba ndugu wa mgonjwa walipie huduma ya matibabu ambayo hutolewa bure.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na hospitali hiyo juzi imeeleza (bila kumtaja mtumishi huyo) kwamba aliomba shilingi 150,000 ili Warioba Joseph Butiku apewe huduma ya mashine ya kumsaidia kupumua.

“Hospitali inakiri kumpokea mgonjwa huyo tarehe 7/8/2026 saa moja usiku akiwa mgonjwa wa rufaa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Butiama. Baada ya matibabu ya awali na uchunguzi wa kimatibabu, alihamishiwa kuendelea na matibabu kwenye Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU),” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kulingana na taarifa hiyo, gharama za matibabu ya mgonjwa huyo zilikuwa zimelipwa kwa mujibu wa taratibu za malipo ya serikali na sehemu nyingine zilitolewa kwa msamaha wa muda.

Hivyo, baada ya kuona malalamiko kwenye mitandao ya kijamii kwamba ndugu wa mgonjwa huyo wameombwa fedha kwa ajili ya mashine ya kumsaidia kupumua - jambo ambalo ni “kinyume cha taratibu kwani huduma hiyo hailipiwi”, hospitali hiyo imetangaza kuchukua hatua dhidi ya mtumishi huyo.

“Yamefanyika mahojiano na ndugu wa mgojwa kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa na kumtambua mtumishi aliyehusika na tukio hili, ambaye atachukuliwa hatua kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma na zile za kitaaluma.

“Aidha, tukio hili limeripotiwa kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa ajili ya uchunguzi na hatua zaidi,” imeeleze taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa hospitali hiyo, Judith Vincent Machumu.

Muhimu: Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Kwangwa imetumia nafasi hiyo pia kuendelea kuwakumbusha wagonjwa na ndugu zao kuwa malipo yote hufanyika kwenye dirisha la malipo kupitia Namba ya Malipo (Control Number) tu.

“Endapo utapata changamoto usisite kuwasiliana na uongozi wa hospitali kupitia namba [za simu] zilizowekwa kwenye [mbao za] matangazo na zinazoonekana kwenye runinga hospitalini hapo,” taarifa hiyo imesisitiza.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages