
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa pili kushoto), akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (kushoto) na viongozi wengine mjini Musoma leo.
Musoma
-------------
Serikali mkoani Mara imiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanzisha mamlaka maalum ya uhifadhi wa Ziwa Victoria kwa uendelevu wa chanzo hicho cha maji ambacho ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amewasilisha ombi hilo leo Agosti 11, 2026 kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ambaye ameanza ziara ya siku nne mkoani Mara.
Kanali Mtambi amesema kutokana na shughuli za kiuchumi na kijamii zinazofanywa ndani ya Ziwa Victoria ipo haja ya kuwa na mamlaka maalum itakayolisimamia ili shughuli hizo ziweze kufanyika kwa ufanisi na kuleta tija zaidi bila kuathiri uhai wake.
Ametolea mfano ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ambao umepata mapokeo makubwa mkoani Mara baada ya serikali kuanza kuwezesha wavuvi, ambapo vijana wengi wameamua kujiajiri kupitia ufugaji huo ndani ya ziwa hilo.
"Kuhusu gharama za uendeshaji hili sio tatizo kwani mamlaka hiyo itakuwa na uwezo wa kujiendesha yenyewe kama zilivyo mamlaka zingine, kikubwa tuwe na chombo ramsi kwa ajili ya kusimamia hii rasilimali yetu muhimu," amesema Kanali Mtambi.
Ameongeza kuwa licha ya Ziwa Victoria kuwa kichocheo muhimu kwa ukuaji wa uchumi bado linakabiliwa na changamoto nyingi, hivyo ni vema kuwa na chombo maalum kitakachosimamia na kupanga namna nzuri ya kufanya shughuli za kiuchumi ndani ya ziwa hilo.

Sehemu ya viongozi na watumishi wengine waliohudhuria kikao hicho
Mkuu wa Mkoa pia ameomba uimarishaji wa sekta ya mifugo, hususan kusaidia upatikanaji wa mbegu bora za kisasa ili kuwasaidia wafugaji waweze kufuga kisasa na kwa tija.
Kanali Mtambi amesema licha ya mkoa wa Mara kuwa na mifugo mingi bado wafugaji hawajapata tija kutokana na kutumia mbegu za asili.
"Tunaomba tupate mbegu bora ambazo mfugaji atapata tija kwa muda mfupi. Mfano kuna ng'ombe ana miezi tisa lakini anakuwa na kilo 1,000 tofauti na hawa tulionao ambapo ng'ombe ana miaka mitatu hadi mitano lakini hawezi kufikisha kilo 1,000," amesema.
Ameongeza kuwa suala la uanzishwaji na ufufuaji wa viwanda, hasa vya kuchakata mazao ya mifugo pia ni la muhimu kwani litasaidia kuboresha mnyororo wa thamani katika sekta ya mifugo.
"Viwanda vitasaidia kuongeza thamani ya mazao ya mifugo kama nyama, maziwa na Ngozi, tunaomba hili nalo lipewe kipaumbele na wizara ili maendeleo yaweze kuwagusa wananchi moja kwa moja," amesema Kanali Mtambi.
Akijibu maombi hayo, Waziri Bashiru amesema tayari yaneanza kufanyiwa kazi lengo likiwa ni kuboresha na kuimarisha sekta za uzalishaji ili kuboresha uchumi wa wananchi, ikiwa pia ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025/50.
"Tuna kituo cha kupandikiza mbegu bora za mifugo kule Arusha na tuna mpango wa kuanza kufungua matawi sehemu mbalimbali nchini ili mbegu hizo ziweze kupatikana kwa urahisi kwa wafugaji waweze kufanya ufugaji wenye tija," amesema Waziri Bashiru.
Kuhusu mamlaka ya usimamizi wa Ziwa Victoria, Waziri huyo amesema wizara yake iko katika hatua nzuri ya uanzishwaji wa mamlaka ya kuhifadhi na kusimamia sekta ya uvuvi ambayo pia itasaidia kulinda maliasili za nchi sambamba na kuboresha shughuli za uvuvi.
Katika hatua nyingine, Waziri Bashiru amaeupongeza uongozi mkoa wa Mara kwa namna ulivyofanya uhamasishaji uliowezesha vijana wengi kuomba mkopo kufuatia shilingi bilioni 200 zilizotengwa kwa ajili ya mikopo kwa vijana nchini.
Amesema Mara ni miongoni mwa mikoa iliyoongoza kwa kutuma maombi mengi ya mikopo hiyo, huku akitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wakuu wa mikoa mingine kuiga mfano huo ili vijana wengi waweze kuomba mikopo hiyo.
"Kwa kweli maombi kutoka Mara ni mengi mno, mmefanya vizuri sana, lakini kuna baadhi ya mikoa maombi ni machache sana hadi tunafikiria kuanza mchakato upya. Nawaagiza wakuu wa mikoa wengine kujifunza kwa mkoa huu," amesema Waziri Bashiru.
No comments:
Post a Comment