
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, SACP Pius Lutumo.
Mara Online News
------------------------
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara limewatia mbaroni walimu sita wa Shule ya Sekondari Makongoro wilayani Bunda, kwa tuhuma za kumpiga na kumsababishia kifo mwanafunzi wao wa kidato cha sita, Peter Marire (23).
Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Mara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Pius Lutumo, ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu leo Ijumaa kwamba walimu hao wanahojiwa kuhusu kifo hicho kilichotokea Agosti 19, 2026 saa tano asubuhi.
RPC Lutumo amesema watuhumiwa hao wanaweza kufikishwa mahakamani siku na wakati wowote mara baada ya Jeshi la Polisi kukamilisha uchunguzi.
Uchunguzi huo unatarajiwa pia kusaidia kubaini chanzo halisi cha kifo cha Marire na iwapo kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu katika utoaji wa adhabu shuleni.
Kifo hicho kinahusishwa na adhabu ya viboko aliyopewa mwanafunzi huyo kwa madai ya kuanguka mtihani wa majaribio, ambapo inadaiwa kuwa alichapwa na walimu hadi akazimia na hatimaye kupoteza maisha.
Inaelezwa kuwa baada ya wanafunzi wenzake kuona hali yake inaendelea kuwa mbaya walimpeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda siku hiyo, ambapo alichunguzwa na kugundulika kuwa alikuwa ameshapoteza uhai.
Taarifa zaidi zinadai kuwa wakati akiendelea kuchapwa, Marire aliwaomba walimu wamuache huku akilalamika kuwa alikuwa akijihisi vibaya na kuishiwa nguvu, lakini walimpuuza na kuendelea kumwadhibu hadi alipozimia.
Tukio hilo limeibua mjadala mpana kuhusu matumizi ya adhabu za viboko shuleni, wajibu wa walimu kulinda usalama na afya ya wanafunzi, pamoja na umuhimu wa kuchukua hatua za haraka pale mwanafunzi anapoonesha dalili za kuugua au kupoteza fahamu.
No comments:
Post a Comment