NEWS

Wednesday, 12 August 2026

Waziri Bashiru azindua miradi ya maendeleo Butiama, Bunda



Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (aliyevaa kizibao cheusi) akishirikiana na wananchi kupiga makofi mara baada ya kuzindua vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Kenkyombo katika wilaya ya Butiama mkoani Mara jana.

Na Godfrey Marwa
Butiama na Bunda
------------------------

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, akiwa amefuatana na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameendelea na ziara yake ya kukagua, kuweka mawe ya msingi, kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi mkoani humo.

Akiwa wilayani Butiama jana Jumatano, Agosti 12, 2026, Waziri Bashiru aliweka jiwe la misingi katika nyumba ya makazi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo inayojengwa kwa gaharama ya shilingi milioni 220.

Waziri Bashiru akikata utepe kuzindua mradi wa ujenzi wa nyumba ya makazi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama

Pia, Waziri Bashiru aliweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Amali ya Musuguri unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.6.

"Wilaya hii [Butiama] ina historia katika uongozi wa nchi yetu akiwemo Mwalimu Julius Nyerere kwa kutujengea uongozi imara. Alifanya kazi kubwa kwa kutuunganisha na kuwa na taifa imara lenye mshikamano.

"Wito wangu kwa wana-Mara ni ninyi kuwa mfano katika taifa letu kwa kudumisha amani, uzalendo, udugu, umoja na mshikamano wa kitaifa. Endeleeni kulinda amani na utulivu, hii ni sifa mliyojijengea.

"Tumuunge mkono Rais wetu [Dkt. Samia Suluhu Hassan] anayeendeleza maono ya Baba wa Taifa kwa kuwekeza kwenye elimu kwa kujenga vyuo hapa,” Waziri Bashiru aliwambia wana-Mara.

Kwa upande wa Bunda, Waziri Bashiru alizindua mradi wa vyumba vya madarasa na vyoo katika Shule ya Msingi Kenkyombo uliotekelezwa kupitia mradi wa Boost kwa shilingi milioni 132.

Waziri Bashiru akisalimiana na wanafunzi alipokwenda kuzindua vyumba vya madarasa na vyoo katika Shule ya Msingi Kenkyombo.

Kisha, Waziri huyo aliweka jiwe la msingi katika mradi wa jengo la Zahanati ya Rubana uliotekelezwa kwa ufadhili wa TANAPA kwa shilingi milioni 122.

Alitumia fursa hiyo pia kuzielekeza halmashauri zote kuelekeza fedha za mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani katika miradi yenye tija, ikiwemo ufugaji wa samaki kwenye vizimba ili kuwezesha vijana wanajikwamua kiuchumi.

“Niwaombe halmashauri, zile asilimia sasa zimeongezeka, mikopo hiyo ielekezwe kwenye maeneo yenye tija, ikiwemo ufugaji wa samaki kwenye vizimba,” alielekeza.
Waziri Bashiru akizungumza na wananchi wilayani Butiama. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi. (Picha zote na Mara Online News)

Aidha, Waziri Bashiru alijibu maswali yaliyoulizwa na wananchi kuhusu kero mbalimbali, ikiwemo za ukosefu wa majosho ya mifugo, migogoro ya wakulima na wafugaji, na ukosefu wa maji.

"Tutaendelea kutenga ardhi na kuweka huduma za mifugo, majosho tunayo yanahitaji kukarabatiwa na kujengwa mapya na fedha kutengwa, kuajiri maafisa mifugo na kuwapa vitendea kazi, Pamoja na kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji kwa amani na upendo.

"Bajeti ya Wizara ya Maji imeongezwa, Bunda wataweza kuchimbiwa malambo ya mifugo na visima virefu ili kutatua changamoto ya maji,” alisema Waziri Bashiru.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages