
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kulia) akimkabidhi Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Chomete, Tuzo ya Mdau Shupavu katika hafla iliyofanyika mjini Tarime jana Jumanne. Katikati aliyevaa shati la madoadoa ni mfanyabiashara Nicholaus Mgaya "Chichake".
Tarime
--------------
Wadau mbalimbali wa maendeleo katika mkoa wa Mara wametunukiwa Tuzo za Mdau Shupavu zinazotolewa na Taasisi ya Holysmile.
Hafla ya kukabidhi tuzo hizo ilifanyika usiku wa kuamkia leo Jumatano, Septemba 30, 2026 katika ukumbi wa Blue Sky, mjini Tarime.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Holysmile, Arnold Bweichum, tuzo hizo zimetolewa kutambua mchango wa wadau hao na kuunga mkono shughuli zao ambazo zinachochea maendeleo ya jamii mkoani Mara.
"Lengo la tuzo hizi ni kutambua mchango wa wadau mbalimbali ndani ya mkoa na pia kuwatia moyo ili waendelee na shughuli zao ambazo ni chachu ya maendeleo yao wenyewe na mkoa wa Mara kwa ujumla," alisema Bweichum.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowelle, ambaye naye alitunukiwa tuzo.

Ukataji wa keki katika hafla hiyo
Meja Gowele aliipongeza Taasisi ya Holysmile kwa kutambua mchango wa wadau hao na kuwatunuku tuzo.
"Nafarijika sana kuona mnatambua michango ya wadau mbalimbali. Ninawapongeza washindi wote na mjue kwamba hamjashinda kwa bahati bali ni kutokana na juhudi na vipaji vyenu," alisema.

Sehemu ya washindi wa tuzo hizo wakifurahia picha ya pamoja
Wadau wengine waliotunukiwa tuzo hizo ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Chomete, mfanyabiashara Nicholaus Mgaya “Chichake”, mwandishi wa habari Frankius Cleophace na CMG Hotels.
Jumla ya tuzo 62 zilikabidhiwa kwa washindi kutoka sekta mbalimbali mkoani Mara.
Hafla hiyo iliwakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta tofauti, ambapo pia walipata fursa ya kufahamiana na michango yao katika maendeleo ya jamii.

No comments:
Post a Comment