NEWS

Wednesday, 30 September 2026

NGOs Mara zakutana Jukwaa la Mwaka 2026, RC Mtambi azitaka kutanguliza uzalendo, maslahi ya taifa



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi (katikati waliokaa), katika picha ya pamoja na viongozi wa NGOs mjini Musoma jana Jumanne wakati wa Jukwa lao Mwaka 2026.

Na Godfrey Marwa
Musoma
--------------

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi, ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kutanguliza uzalendo na maslahi ya taifa yanapotekeleza shughuli za kijamii.

Pia, ameyashauri kubuni vyanzo vya mapato kwa ajili ya kujiendesha badala ya kutegemea mashirika ya kigeni pekee.

Mtambi aliyasema hayo mjini Musoma jana Jumanne katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa Jukwaa la Mwaka la NGOs za mkoani Mara, ambazo ziliwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli zao kwa mwaka 2026.

Lengo lilikuwa kueleza changamoto za mashirika hayo na namna ya kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utekelezaji wa shughuli zao.

Sehemu ya washiriki wa mkutano huo wakifurahia jambo

“Pendeni nchi yenu, hakikisheni mnayoyafanya mnatanguliza maslahi ya taifa lenu, mlinde maslahi ya Mtanzania kwa kufuata sheria, kuheshimu mila na desturi za Kitanzania kwa ustawi wa taifa.

“Baadhi ya mashirika yamekuwa yakiendeshwa kwa usiri mkubwa. Niwatake muendeshe shughuli zenu kwa uwazi kwa kupanga mipango inayoendana na ya serikali na dira ya taifa," alisema Brigedia Jenerali Mtambi na kuongeza:

“Tafuta wafadhili wa ndani, tubuni mifumo ya kidijitali kupata rasilimali fedha kusaidia uendeshaji wa shughuli zenu, kukoma kutegemea wafadhili wa nje pekee. Ibueni maeneo kwa kuanzisha afua za kupunguza makali ya maisha ya wananchi.”

Viongozi wa dini (kushoto) pia walishiriki mkutano huo

Kwa upande wake Mjumbe Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Rhobi Samwelly ambaye pia ni Mkurugenziwa wa Shirika Hope for Girls and Women in Tanzania, alisema NGOs ni wameendelea kuwa washirika wa serikali katika kuchochea maendeleo ya jamii.

“Tunaomba serikali na wadau wetu wa maendeleo kutushirikisha katika mipango ya serikali, mazingira wezeshi yanayoruhusu kuchangia kikamilifu katika dira ya maendeleo ya taifa ya 2050,” alisema Rhobi.

Brigedia Jenerali Mtambi (katikati), Rhobi Samwelly (kulia) na viongozi wengine wakipiga makofi kufurahia jambo katika mkutano huo. (Picha zote na Mara Online News)

Jukwa hilo la NGOs lilikuwa na kaulimbiu inayosema “Fikira Mpya kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha kupitia Vyanzo vya Ndani”.

Lilizikutanisha NGOs 146 na kuhudhuriwa na wadau wa maendeleo, wawakilishi sekta binafsi, taasisi za fedha, viongozi wa dini na wawakilishi wa NaCoNGO kutoka wilaya za mkoa wa Mara na taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages