NEWS

Friday, 2 October 2026

Barrick North Mara wakabidhi mradi wa maji Kewanja



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (katikati aliyevaa kofia), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali na wananchi wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji kijijini Kewanja jana.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
-------------

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara umekabidhi rasmi mradi wa upanuzi wa chanzo na usambazaji wa majisafi na salama utakaonufaisha maelfu ya wananchi katika kijiji cha Kewanja kilichopo jirani na mgodi huo.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, alipokea na kuzindua awamu ya pili ya mradi huo ambao umegharimu shilingi bilioni 2.66, jana Alhamisi, Oktoba 1, 2026.

Mradi huo umetekelezwa chini ya mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) wa mgodi huo ambao unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele, akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa mradi huo

Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na Meneja wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko katika hafla ya makabidhiano hayo, kukamilika kwa mradi huo kutaongeza idadi ya wanufaika kutoka 27,742 (awamu ya kwanza) hadi 125,566.

“Leo tunakabidhi awamu ya pili ya mradi ambayo inahusisha kilomita 5.5 za bomba kuu la kusafirisha maji na kilomita 8.6 za mtandao wa usambazaji katika kijiji cha Kewanja,” alisema Lyambiko.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo ni hatua muhimu katika kuboresha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi wa vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa North Mara.

“Kwetu kama mgodi, maji ni zaidi ya huduma, ni rasilimali muhimu inayogusa maisha, afya, uchumi na ustawi wa wananchi. Tunajivunia kuwa sehemu ya juhudi za serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama,” alisema Lyambiko.

Alisema tangu mwaka 2019 Barrick North Mara imekuwa ikitenga wastani wa shilingi bilioni nne kila mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo ya maji, elimu, afya, miundombiunu ya barabara, mazingira na uwezeshaji kiuchumi hasa kwa vijana.

Viongozi wakishangilia uzinduzi wa mradi huo kijijini Kewanja

Awali, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Tarime, Mhandisi Leo Respicius, alisema maji ya mradi huo yamethibitishwa na vipimo vya kitaalamu kuwa ni safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

“Kukamilika kwa mradi huu ni ushuhuda mwingine wa jinsi mgodi wa Barrick North Mara unavyotekeleza azma yake ya kuwa mshirika wa maendeleo kwa jamii inayozunguka mgodi na wilaya ya Tarime kwa ujumla,” alisema.

Meja Gowele akimtwisha kisha kumtua mkazi wa kijiji cha Kewanja ndoo ya maji

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Gowele, aliushukuru Mgodi wa Barrick North Mara kwa kuendelea kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kijamii kwa vitendo kupitia mpango wake wa CSR.

“Tumefurahi kuzindua huu mradi wa maji hapa. Niwapongeze na kuwashukuru Barrick kwa namna ambavyo inashirikiana na serikali kutekeleza miradi ya kijamii kupitia mpango wao wa CSR,” alisema.

Meja Gowele alisema utekelezaji ya miradi hiyo unaenda sambamba na maelekezo ya Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. “Mhe. Rais Samia anataka huduma ya maji kwa wananchi ifike kila kona,” alisisitiza.

Aliwataka wakazi wa kijiji cha Kewanja kutunza mradi huo ili uwe endelevu kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.

Aidha, Meja Gowele aliwasihi wananchi wanaozunguka mgodi wa North Mara kuendelea kuunga mkono mgodi huo ili waendelee kufurahia na kunufaika zaidi na uwekezaji huo.

Viongozi wakifurahia uzinduzi wa mradi huo

Naye Diwani wa kata ya Kemambo kilipo kijiji cha Kewanja, Rashid Bogomba, aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na kuboresha mahusiano mema na Mgodi wa Barrick North Mara.

“Kitu kama hiki [mradi huo wa maji] tungekisubiri kwa miaka mingi lakini leo tumekipata kwa urahisi kupitia Mgodi wa Barrick North Mara. Tuendelee kuwapa ushirikiano watu wa Barrick na hii itatusaidia sana,” alisema Bogomba ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) ya Barrick North Mara.

Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime nao walionesha kufurahishwa na mradi huo wa maji na mingine inayotekelezwa na mgodi huo kupitia mpango wake wa CSR.

“Tumefurahishwa sana na mradi huu na tunatambua kazi nzuri inayofanywa na kampuni ya Barrick.ama halamshauri tutaendelea kuwapa ushirikiano mzuri,” alisema Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Juster Magabe.

Nao wananchi na viongozi wengine wa kijamii waliohudhuria halfa hiyo walisema mradi huo utawaondoa adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji katika vyanzo ambavyo sio salama na uhakika.

Kufika kwa maji karibu na makazi ya wananchi kunawapunguzia wanawake adha ya kutembea umbali mrefu, na hivyo kupata muda wa kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na kukuza uchumi wa kaya.

Viongozi wa Barrick North Mara (kushoto) na wafanyakazi wa RUWASA (kulia) wakipiga makofi kuunga mkono maelekezo ya Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele (katikati), wakati wa makabidhiano na uzinduzi wa mradi huo. (Picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages