NEWS

Friday, 2 October 2026

Tarime: Benki ya CRDB yakabidhi msaada wa madawati Shule ya Msingi Mapinduzi



Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl. Saul Mwaisenye (aliyevaa shati jeupe), akipokea madawati kutoka Benki ya CRDB na kuyakabidhi kwa Shule ya Msingi Mapinduzi iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime leo Oktoba 2, 2026.

Na Godfrey Marwa
Tarime
--------------

Benki ya CRDB Tawi la Tarime kupitia programu yake ya Keti Jifunze, imekabidhi msaada wa madawati 40 ya wanafunzi kwa Shule ya Msingi Mapinduzi iliyopo Halamashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika leo Oktoba 2, 2026 na kuongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Tarime, Mwl. Saul Mwaisenye, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele.

DAS Mwaisenye ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuendelea kuwa mdau mkubwa katika maendeleo ya elimu, huku akiwataka wanafunzi kuyatunza kwa manufaa endelevu ya shule hiyo.

Sehemu ya madawati yaliyotolewa na Benki ya CRDB

"CRDB ni wadau wakubwa wa maendeleo ya elimu kupitia kampeni yao Keti na Ujifunze, tunashukuru kutushika mkono kwa kutuletea dawati, tutaendelea kuwaunga mkono.

"Mahitaji tunayo makubwa, wadau wengine waige jambo hili. Wanafunzi tunawataka muyatunze haya madawati ili wadogo zenu waje wayatumie,” amesema Mwaisenye.

DAS Mwaisenye, wanafunzi na walimu wakifurahia kupokea madawati hayo.

Awali, Kaimu Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Glory Mponzi, amesema benki hiyo inatoa msaada wa madawati kutokana na asilimia 10 ya faida inayopata ili kuunga mkono jamii na serikali katika kuboresha mazingira ya kusomea.

"Tunagawa madawati kusaidia serikali kuwa na taifa la wasomi na elimu bora. Tunawasihi watoto wetu wayatunze hayo madawati. Mkiwa wakubwa msisahau benki yetu [CRDB], muwe mabalozi. Tukipata faida asilimia 10 tunaleta kwenu kama asante.

"Tunawaomba wadau waendelee kutumia benki yetu ili tuendelee kukuza mtaji na kupata faida ambayo mwisho wake asilimia kumi tunairudisha kwa jamii,” amesema Mponzi.

Kaimu Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Glory Mponzi (kulia) na Meneja wa benki hiyo Tawi la Tarime, Hansi Kalinga, wakifurahia picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wakati wa hafla hiyo.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mapinduzi, Lucy Lucas Akyoo, ameishukuru benki hiyo kwa msaada huo wa madawati akisema yatawapunguzia changamoto iliyokuwepo.

"Tunashukuru CRDB wametusaidia kupunguza tatizo la wanafunzi kukaa chini kwa asilimia kubwa. Pia ikiwapendeza watusaidi mashine ya photocopy ili kupandisha ufaulu,” alisema Mwl. Akyoo.

Naye Afisa Elimu Aawali na Msingi Halimashauri ya Mji wa Tarime, Mwl. Shabani Mangosongo, ameishukuru Benki ya CRDB na serikali kwa namna wanavyoshirikiana kuboresha mazingira ya elimu katika wilaya hiyo.

Mgeni rasmi, DAS Mwaisenye (aliyevaa shati jeupe), wafanyakazi wa Benki ya CRDB na walimu wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa hafla ya makabidhiano ya madawati hayo. (Picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages