NEWS

Wednesday, 7 October 2026

Kampuni 14 kuongeza fursa sekta ya madini kwa kuanzisha miradi mipya



Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

Na Mwandishi Wetu
Geita
------------

Fursa katika sekta ya madini zitaongezeka na kupanuka zaidi kutokana na kampuni 14 zinazotarajiwa kuanzisha miradi mikubwa pamoja na leseni 28 za uchimbaji wa madini ya kinywe.

Kwa mujibu wa Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, fursa hizo zitawagusa wazawa chini ya Sera ya Ushirikishwaji Watanzania katika kuharakisha kasi ya ukuaji wa uchumi.

Waziri Mavunde alisema hayo hivi karibuni mkoani Geita wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ushirikishwaji Watanzania katika Sekta ya Madini yaliyokwenda sambamba na Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini.

Alisema serikali tayari imewataka wamiliki wa leseni za madini ya kinywe kuharakisha utekelezaji wa miradi yao.

Alizitaka kampuni za Kitanzania kuunganisha mitaji, vifaa, teknolojia na utaalamu ili kushindania kazi kubwa zinazohitaji uwezo mkubwa wa kifedha na ufundi.

Mavunde alisema serikali inalenga kuhakikisha kuwa asilimia 90 ya shilingi trilioni 5.1 zinazotumika kila mwaka kununua bidhaa na huduma katika sekta ya madini zinabaki nchini kupitia Sera ya Ushirikiishwaji wa Watanzania.

Lengo la sera hiyo ni kuhakikisha sekta ya madini inaacha manufaa mapana katika uchumi wa Tanzania.

Serikali ya Tanzania imeweka mazingira wezeshi kwa wazawa kushiriki katika ugavi wa bidhaa ba huduma, ajira, uongozi wa kampuni za madini, utafiti na hatua-kwa-hatua uzalishaji wa bidhaa zinazotumiwa na migodi.

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, kati ya ajira rasmi zaidi ya 19,000 katika sekta ya madini, asilimia 96 zinashikiliwa na Watanzania, huku idadi ya wataalamu wanaoshika nafasi za juu za kitaalamu na uongozi katika kampuni za madini ikiongezeka ili kuimarisha sera ya ushirikishwaji.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages