NEWS

Monday, 5 October 2026

Leseni za Barrick North Mara zahuishwa kwa miaka 15 zaidi



Lori likiwa kazini katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara

Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
-----------------------

Kampuni ya kimataifa ya uchimbaji madini, Barrick Mining Corporation, imetangaza kuwa Serikali ya Tanzania imehuisha Leseni zake Maalumu za Uchimbaji (Special Mining Licenses) katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa miaka mingine 15 ijayo.

Taarifa iliyotolewa na Barrick jijini Dar es Salaam Oktoba 5, 2026, imesema kuhuishwa kwa leseni hizo kunamaanishwa kuwa uwekezaji utaendelea katika Mgodi wa North Mara kwa wafanyakazi wake na jamii zilizo jirani kwa muda mrefu.

Tangu Barrick ilipochukua usukani wa kuuendesha mwaka 2019, mgodi wa North Mara uliopo wilayani Tarime, Mara, umeongeza ajira kwa wazawa, kupanua wigo wa kiuchumi na kuimarisha uhusiano na jamii zinazouzunguka.

Kwa sasa, asilimia 96 ya wafanyakazi wa migodi ya Barrick ya North Mara na Bulyanhulu uliopo Kahama, Shinyanga, ni Watanzania wapatao 3,000, huku asilimia 47 ya hao wakitoka katika jamii zinazozunguka migodi hiyo.

Barrick imeingiza takriban dola za Marekani bilioni 5.3 katika uchumi wa Tanzania tangu mwaka 2019, zikiwemo dola bilioni 1.2 kwa mwaka 2025 pekee, kupitia kodi, mrabaha, mishahara, gawio na ununuzi kutoka kwa wazabuni wa ndani.

Ushiriki wa wazawa unabaki kuwa msingi mkuu, huku asilimia zaidi ya 90 ya manunuzi yakifanywa kutoka kwa kampuni zilizosajiliwa Tanzania, nyingi zikiwa ni ambazo zinamilikiwa na Watanzania.

Mwaka 2025, Barrick ilitambuliwa na Serikali ya Tanzania kwa kutunukiwa tuzo kadhaa, zikiwemo za kuwa mlipaji mkubwa wa gawio na mchangiaji mkubwa katika mapato ya serikali.

“Hii ni hatua muhimu kwa mgodi wa North Mara na kwa ubia wetu na Serikali ya Tanzania,” amesema Seb Bock, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa shughuli za Barrick duniani.

“Tangu mwaka 2019, tumekuwa tukifanya kazi na Serikali ya Tanzania na jamii za wenyeji kujenga ushirikiano imara na kutengeneza fursa zaidi kwa Watanzania wote.

“Msingi wa shughuli zetu ni kujenga ushirikiano wa kina na wa kuaminiana na wadau wote, na uhuishaji huu wa leseni unaakisi dhamira hiyo,” amesema Seb.

Barrick na Serikali ya Tanzania walianzisha kampuni ya Twiga Minerals mwaka 2019 ili kuendesha kwa pamoja migodi ya North Mara na Bulyanhulu.

Serikali inamiliki asilimia 16 ya hisa katika kila mgodi, na washirika hao wawili hugawana faida kwa usawa.

Kamati za Maendeleo ya Jamii katika maneo hayo husaidia kuamua miradi gani ipewe kipaumbele, kama vile shule, zahanati na barabara.

“Mahusiano katika Mgodi wa North Mara yameimarika tangu Barrick ilipochukua hatamu ya kuuendesha. Kwa sasa, wananchi wanauona mgodi huo kama mshirika wa jamii,” amesema Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele.

Barrick ni kampuni ya kimataifa inayojishughulisha na utafutaji, uchimbaji madini na maendeleo katika nchi 17 duniani.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages