
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa.
Mara
-----------
Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, chini ya Mwenyekiti Patrick Chandi Marwa, kwa kushirikiana na Kamati ya Uratibu, umeandaa kikao maalum kitakachojadili fursa za kiuchumi zilizopo mkoani na namna bora ya kuzitumia kuinua uchumi wa wananchi, mkoa na taifa kwa ujumla.
Kikao hicho ambacho kaulimbiu yake ni “Fursa ni Uchumi”, kitafanyika Alhamisi, Oktoba 8, 2026, katika ukumbi wa CMG Hotels, Tarime kuanzia saa nane mchana.
Kinatarajiwa kujenga ushirikiano kati ya sekta ya umma, binafsi na wadau wengine wa maendeleo katika kutambua fursa, kuondoa vikwazo vinavyoweza kuzuia uwekezaji na kuweka mazingira yanayowezesha wananchi kunufaika zaidi na rasilimali na fursa zilizopo.
Watu zaidi ya 100 wanatarajiwa kushiriki katika kikao hicho ili kujenga mtazamo wa pamoja kuhusu mwelekeo wa maendeleo ya mkoa wa Mara, hususan katika kuweka mikakati, kuibua maeneo yenye uwezo wa kuzalisha ajira, kuongeza kipato cha wananchi na kukuza shughuli za kiuchumi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, aliliambia Gazeti la Sauti ya Mara jana kwamba maandalizi ya kikao hicho yamekamilika.
“Hiki ni kikao muhimu kwa ajili ya kujadili fursa za kiuchumi na maendeleo ya mkoa wa Mara na kuwaunganisha wadau wa maendeleo,” alisema Chandi.
Mkoa wa Mara umebarikiwa kuwa na rasilimali mbalimbali ambazo zikitumika vizuri zinaweza kusaidia kuharakisha na kuleta maegeuzi makubwa ya kiuchumi katika mkoa huo.
Rasilimali hizo ni pamoja na uwepo wa sehemu kubwa wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na mapori ya akiba yenye utajiri mkubwa wa wanyamapori, madini, mifugo na ardhi ambayo inastawisha mazao mbalimbali ya kibiashara na chakula kama vile mahindi, mtama, mihogo, pamba, tmbaku na kahawa aina ya Arabica ambayo inafanya vizuri katika soko la dunia.
Pia, mkoa wa Mara ambao unapakana na mataifa ya Afrika Mashiriki ya Kenya na Uganda, umejaaliwa kuwa na sehemu kubwa ya Ziwa Victoria na hivyo kuufanya pia kuwa moja ya mikoa ya Kanda ya Ziwa inayozalisha samaki aina ya sato kwa wingi.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment