
Salim Mwanyenza akicheza katika Uwanja wa Gofu Serengeti hivi karibuni
cgmjournalist@gmail.com
---------------------------------
Wakati mchezo wa gofu unaohusishwa na matajiri, viwanja vya kifahari na vifaa vya gharama kubwa, kuna simulizi ya kipekee inayorejesha mjadala kwenye jambo la msingi zaidi; kipaji, nidhamu na uthubutu wa kuanza pale ulipo.
Simulizi hiyo siyo nyingine, ni ya Salim Mwanyenza, aliyeweka historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza mcheza gofu mahiri wa kulipwa katika ngazi ya kimataifa.
Mwanyenza alianza kwa kubeba vifaa vya wachezaji akiwa mtoto, lakini hakubaki kuwa mtazamaji wa ndoto za wengine.
Safari yake katika mchezo wa gofu ni simulizi ya uvumilivu, kujifunza, mafanikio na urithi unaoendelea kuishi, ikiwemo mchango wake wa kuchora ramani ya Uwanja wa Gofu Serengeti wenye hadhi ya kimataifa.
Mwanyenza, ambaye alizaliwa mwaka 1943 mkoani Tanga, alianza safari yake hiyo mwaka 1956 kwa kubeba mizigo ya wachezaji wa gofu katika Klabu ya Gymkhana Tanga.
Historia yake inaakisi maneno ya wahenga kwamba fursa inaweza kuanza katika nafasi ambayo wengine hawaioni kuwa na thamani kubwa.
Akizungumza na Gazeti la Sauti ya Mara hii hivi karibuni katika Uwanja wa Gofu uliojengwa katika eneo la Fort-Ikoma, pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mwanyenza anasema ubebaji vifaa vya wacheza gofu kwake ulikuwa darasa lisilo rasmi la mchezo huo ambao baadaye ulibadilisha maisha yake.
Alipata fursa ya kuushuhudia, kufahamu mazingira yake na kujenga uzoefu wa shughuli za gofu kabla hata hajaanza kuucheza kitaalamu.
Ni safari iliyobeba ujumbe muhimu kuhusu maendeleo ya vipaji. Wakati mwingine, mtu haanzi kwa kuwa mchezaji, bali kwa kuwa karibu na mchezo, kujifunza na kutambua siri ya mafanikio yake.
Miaka ilisonga, Mwanyenza akaendelea na safari yake ya elimu. Anasema mwaka 1969, alihitimu darasa la 12 huko Tanga. Baadaye alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kabla ya kuingia rasmi katika mafunzo ya gofu.
Mwaka 1970, alijiunga na Klabu ya Gofu Gymkhana Tanga kwa lengo la kujifunza kucheza mchezo huo.
Kijana aliyekuwa akibeba mizigo ya wachezaji sasa akawa mwanafunzi wa gofu, akijifunza mbinu na kanuni za mchezo ambao ulimvutia muda mrefu.
“Julai 1977, nilianza kucheza gofu kwa kulipwa, huku pia nikifundisha mchezo huo,” anasema Mwanyenza ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 83.
Aidha, nafasi yake ya kufundisha, anasema ilimpa fursa ya kuendeleza ujuzi wake na kuwasaidia wengine kujifunza mchezo huo.
Wakati mwingine, mafanikio hayaji kwa lazima kupitia njia ya mkato, bali hujengwa hatua kwa hatua, kwa miaka ya kujifunza, kujituma na kutokata tamaa.
“Nilifanikiwa kushinda misimu miwili mfululizo katika mashindano ya gofu hapa nchini, ilikuwa mwaka 1974 na 1975,” anasema mtaalamu huyo wa gofu.
Mafanikio ya Mwanyenza hayakuishia katika viwanja vya nyumbani. Uwezo wake ulimfikisha katika mashindano ya gofu ya kimataifa ndani na nje ya Afrika.
Anasema ameshiriki mashindano ya gofu katika nchi 16 za Afrika, zikiwemo Kenya, Nigeria, Ghana, Ivory Coast, Zambia, Zimbabwe, Malawi na Mauritius.
“Nje ya bara la Afrika, nilishiriki mashindano ya gofu katika mataifa ya Ufaransa, Norway, Uingereza, Marekani, Jamaica na Dubai,” anasema Mwanyenza.
Safari yake ya kutoka Tanga, Tanzania hadi nchi mbalimbali duniani, anasema ilikuwa fursa ya kukutana na wachezaji wengine, kupima uwezo wake na kuendelea kujifunza katika mazingira tofauti ya ushindani.

Salim Mwanyenza
Mwanyenza anaamini kwamba gofu ndiyo mchezo bora zaidi duniani. “Gofu ndiyo mchezo mzuri duniani,” anasema.
Anataja faida za goku kuwa ni mazoezi ya mwili, kujenga afya, kuburudisha, kukuza uwezo wa mtu kujiamini na ujasiri wa kufanya jambo hata akiwa peke yake.
Kwa mujibu wa Mwanyenza, mtu anaweza kuanza kucheza gofu akiwa mdogo na kuendelea hadi uzeeni, tofauti na michezo mingine ambayo huwa na changamoto kadiri umri unavyoongezeka.
“Gofu unaweza kuanza kucheza ukiwa mdogo mpaka kuingiza kaburini, lakini michezo mingine ukiwemo wa kukimbia huwezi. Pia, unaweza kucheza gofu ukiwa peke yako,” anasema.
Kwa mtazamo wake, angependa kuona na kusikia watu wengi wakijiunga na vilabu vya gofu na kuingia viwanjani kucheza.
Mafanikio ya Mwanyenza yanaonekana pia katika maisha yake nje ya uwanja. Anasema mapato yake kupitia mchezo huo yamemwezesha kujenga nyumba, kumiliki shamba na kusaidia kulipa ada za shule za watoto. “Maisha yangu siyo mabaya,” anasema.
Ushiriki wake ujenzi Uwanja wa Gofu Serengeti
Mwanyenza pia ameweka alama nyingine katika maendeleo ya utalii nchini Tanzania kutokana na mchango wake wa kuchora ramani ya ujenzi wa Uwanja wa Gofu Serengeti.
Uwanja huo ulizinduliwa rasmi hivi karibuni na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ni zao jipya la utalii ambalo limebuniwa na TANAPA ili kuwavutia watalii wanatembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti kukaa zaidi na hivyo kukuza mapato ya utalii kwa maendeleo ya taifa.
Kwa mujibu wa Mwanyenza, alichora ramani ya uwanja huo kwa mfano wa kipepeo. “Hiki kiwanja mimekichora mimi kwa mfano wa butterfly (kipepeo),” anaeleza.
Anasema alishirikiana na mtaalamu wa gofu, Mhandisi Enock Magile, katika ujenzi wa uwanja huo, na kwamba vijana waliopata ajira katika shughuli za ujenzi huo walitoka vijiji jirani.
Kwa Mwanyenza, ambaye amekuwa sehemu ya historia ya gofu kwa muda mrefu, kuhusika katika ujenzi wa uwanja huo ni hatua nyingine ya mchango wake katika maendeleo ya mchezo anaoupenda muda wote.
Anavutiwa kucheza kwenye Uwanja wa Serengeti
Alipoulizwa na Gazeti la Sauti ya Mara kama naye amepata fursa ya kucheza kwenye uwanja huo, Mwanyenza alijibu: “Naachaje kucheza kwenye uwanja mzuri hivi.”
Anafafanua kuwa baada ya ujenzi wa uwanja huo kukamilika, ameendelea kucheza gofu hapo kutokana na upekee wake na hadhi yake ya kimataifa.
Anataja mambo yanayoufanya uwanja huo kuwa wa kipekee. Kwanza, umejengwa katika ardhi tambarare na pili, kuna upepo unaompa mchezaji vikwazo na kumlazimu kujifunza zaidi ili kuboresha uwezo wake.
Katika gofu, uwezo wa mchezaji hautegemei ukakamavu pekee. Unahitaji pia umakini, maamuzi sahihi na uwezo wa kuendana na mazingira ya uchezaji.
Kwa mtazamo wa Mwanyenza, upepo wa Serengeti ni sehemu ya changamoto inayoweza kumjenga mchezaji wa gofu na kuimarisha mbinu zake.
Upekee wa uwanja huo hauishii katika ardhi yake au mazingira ya upepo, bali pia unawapa wachezaji fursa ya kucheza huku wakifurahia kutazama wanyamapori katika mazingira ya asili.
Hivyo, Mwanyenza anaipongeza TANAPA kwa kubuni uwanja huo, akisema ni muunganiko wa michezo na utalii unaoweza kuongeza mvuto wa eneo hilo kwa wageni wanaotafuta uzoefu tofauti.
“Wageni wengi wanaocheza gofu duniani wakisikia kwamba kuna uwanja mzuri ambao wanaweza kucheza huku wakiangalia wanayapori watamiminika hapa,” anasema.
Bado anaamini anaweza kuwashinda vijana
Mwanyenza anasema kwa sasa bado anacheza gofu kama mchezo anaoupenda, ingawa hashiriki tena mashindano kama ilivyokuwa katika miaka yake ya ushindani.
Hata hivyo, anapowatazama wachezaji wa siku hizi, anaamini kuwa akiingia kushindana nao anaweza kuwashinda licha ya umri wake mkubwa.
“Mpaka sasa ninacheza gofu, ila siyo kwa kushindana, lakini vijana wengi nikiona wanavyocheza siku hizi, ninaweza kuwashinda na uzee wangu,” anasema Mwanyenza kwa kujiamini.
Je, gofu ni mchezo wa matajiri pekee?
Kwa muda mrefu, mchezo wa gofu umehusishwa na watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha kutokana na gharama za vifaa, ada za uanachama na matumizi ya viwanja.
Mtazamo huo umekuwa kikwazo kwa baadhi ya watu wanaotamani kuujua mchezo huo, hata kabla hawajapata nafasi ya kujifunza misingi yake.
Lakini Mwanyenza ana mtazamo tofauti. Yeye anaamini kuwa mtu yeyote anaweza kucheza gofu, ilmradi tu afuate sheria zake. “Gofu siyo mchezo wa matajiri, isipokuwa ni kufuata sheria zake,” anasisitiza.
Hamaanishi kwamba changamoto za gharama hazipo, ila anasisitiza kuwa mchezo huo haupaswi kutazamwa kama haki ya kundi fulani la watu. Anasema jambo la msingi ni utayari wa kujifunza na kufuata kanuni za mchezo huo.
Historia ya Salim Mwanyenza mwenyewe ni mfano hai. Alianza kwa kufanya kazi ya kubeba mizigo ya wacheza gofu, baadaye akajifunza kucheza na hatimaye akawa mchezaji wa kulipwa na kushiriki mashindano ya kimataifa.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment