NEWS

Tuesday, 13 October 2026

Serikali yampongeza Nyambari Nyangwine kwa kuwa mfano bora wa uwekezaji katika mataifa mbalimbali



Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo (wa tatu kushoto), akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Nyambari Nyangwine Group of Companies Limited (NNGCL), Nyambari Nyangwine (wa tatu kulia), wakati wa Kongamano la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji, lililofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 11, 2026.

Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
--------------------

Serikali imempongeza mfanyabiashara Nyambari Nyangwine kwa kupanua wigo wa shughuli zake nje ya mipaka ya Tanzania, zikiwemo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Maziwa Makuu, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na mataifa mengine.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, alitoa pongeza hizo jijini Dar es Salaam, Oktoba 11, 2026 wakati akifungua Kongamano la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji lililoambatana na uzinduzi wa vitabu vya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania, vilivyoandikwa na mtoto wa Nyambari Nyagwine, Benson.

Sehemu ya washiriki wa kongamano hilo

Nyambari Nyangwine ni Mwenyekiti wa Nyambari Nyangwine Group of Companies Limited inayojishughulisha na uchapishaji wa vitabu, miongoni mwa biashara nyingine ndani na nje ya Tanzania.

“Ndugu Mwenyekiti, nakushukuru na nakupa pongezi za dhati kwa kuwa mfano wa kampuni ya Kitanzania inayovuka mipaka na kufanya biashara katika nchi za Afika Mashariki, Maziwa Makuu na SADC,” alisema Waziri Akwilapo Ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi.

Waziri Dkt. Akwilapo akizungumza katika kangamano hilo

Dkt. Akwilapo alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaithamini sekta binafsi kama mbia halisi wa maendeleo nchini, ikiamini kuwa hakuna taifa linaloendelea bila sekta binafsi imara.

Kwa mujibu wa Waziri Akwilapo, juhudi za kampuni za Kitanzania kuingia katika masoko ya kimataifa ni mfano kwa vijana na wafanyabiashara wengine wanaotaka kukuza biashara zao huku wakichangia maendeleo ya taifa.

Aliwashukuru waandaaji, hususan NNGCL chini ya Mwenyekiti wake, Nyambari Nyangwine, kwa kuandaa kongamano hilo la kimataifa lililowakutanisha wadau mbalimbali kutoka mataifa tofauti duniani.

Alisema, uwepo wa wafanyabiashara wa ndani na wa kimataifa, taasisi za umma, wadau wa elimu, utamaduni na utalii unatoa fursa ya kujadili masuala ya maendeleo, kuimarisha uhusiano wa kibiashara, kubadilishana uzoefu, kuanzisha ushirikiano, kubainisha maeneo mapya ya uwekezaji na kuweka mikakati ya kutumia rasilimali zilizopo kwa maendeo ya taifa.

Waziri Akwilapo alisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kujenga uchumi wenye ushindani, unaozalisha ajira na kutoa nafasi kwa Watanzania kunufaika na uwekezaji.

Alitumia nafasi hiyo pia kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kutumia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali nchini kwa uwekezaji wenye faida na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.

Sehemu nyingine ya washiriki wa kongamano hilo

Wageni waliohudhuria kongamano hilo ni kutoka Poland, Uturuki, Dubai, China, India, Israel, Burundi, Kenya, Uganda, Zambia, Congo, Indonesia, Qatar na Saudi Arabia, miongoni mwa nchi nyingine ambazo Nyambari Nyangwine anafanya nazo biashara.

Washiriki hao wanawakilisha sekta za uchumi na uwekezaji kama vile usafiri na usafirishaji, utalii, uchapishaji, elimu, kilimo, afya, madini, viwanda, nishati, ujenzi wa majengo na miundombinu, miongoni mwa maeneo mengine.

Katika kongamano hilo, wafanyabiashara wa Tanzania walipata fursa ya kutangaza na kutambulisha bidhaa na huduma zao mbalimbali katika medani ya kimataifa.

Nyambari Nyangwine akizungumza katika kongamano hilo

Nyambari Nyangwine alisema kongamano hilo ni fursa adhimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa Tanzania kukutana na wenzao kutoka mataifa mbalimbali.

Alisema lengo la kongamano hilo ni kuwezesha uanzishwaji wa ubia wa kimkakati, upatikanaji wa mitaji, teknolojia, utaalamu, masoko mapya na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia kama kitovu cha biashara na uwekezaji barani Afrika, kwa kuonesha fursa mbalimbali zilizopo.

Mbali na biashara, Nyambari Nyangwine pia ni mwanasiasa ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mkoani Mara kupitia chama tawala - CCM.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages