
Sehemu ya kiwanda cha wire mesh cha Geofields Tanzania Limited kilichopo Kerege, Bagamoyo mkoani Pwani.
Bagamoyo
-----------------
Tanzaniia imeanza kuzalisha bidhaa zinazotumika migodini kwa shughuli za uchimbaji madini.
Hiyo ni hatua muhimu kwa taifa katika kuongeza ushiriiki wa wananchi kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema hivi karibuni huko Kerege wilayani Bagamoyo, Pwani kuwa lengo la serikali ni kuigeuza Tanzania kuwa kituo cha uzalishaji wa bidhaa na utengenezaji wa vifaa vya migodini barani Afrika.
Waziri Mavunde aliyasema hayo baada ya kuzindua kiwanda cha wire mesh cha Kampuni ya Geofields Tanzania Limited, kupitia Geofields Underground Support (GUS).
Alisema nia ya serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani ili kuongeza uwezo wa kampuni za kizalendo kuzalisha bidhaa na kutoa hudua zinazokidhi mahitaji ya migodi nchini na katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Kuhusu ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini, Waziri Mavunde alisema Sheria ya Madini inaweka masharti ya ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka kampuni za Kitanzania na ushirikiano kati ya kampuni za ndani na za kigeni pale uwezo wa utoaji huduma haujajengeka nchini.

Waziri Mavunde (aliyeelekeza mikono sikioni) akiwa katika kiwanda wire mesh cha Geofields Tanzania Limited
Waziri Mavunde aliiagiza Tume ya Madini Tanzania kushirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)) kukagua kampuni zilizoingia ubia ili kuthibitisha kuwa zinafanya shughuli zilizosajiliwa na kutimiza masharti yanayotakiwa.
Alibainisha kuwa shilingi trilioni 5.1 zilizo kwenye mnyororo wa manunuzi wa sekta ya madini zinahusishwa na kampuni zisizozidi sita na akawahimiza Watanzania kujiandaa kutumia fursa zilizopo kwa kuongeza mitaji.
Kiwanda cha Geofields Tanzania Limited alichozindua Waziri Mavunde kina uwezo wa kuzalisha vipande 100,000 vya wire mesh kwa mwaka, kwa mujibu wa Mwanzilishi na Mkurugenzi wake, Denis Dillip.
Akizungumza kwenye sherehe ya uzinduzi wa kiwanda hicho, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, alisema mkoa huo hivi sasa una viwanda 1,768.
Uzinduzi wa kiwanda cha Geofields Tanzania Limited ni sehemu ya juhudi za kuzalisha bidhaa zitumikazo migodini na kupanua fursa za ajira.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment