NEWS

Sunday, 11 October 2026

Barrick North Mara wajenga shule mpya ya msingi kijijini Kerende



Sehemu ya mbele ya vyumba vya madarasa ya shule mpya ya msingi Mgosi iliyojengwa na Mgodi wa Barrick North Mara kupitia mpango wake wa CSR.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
-------------

Kijiji cha Kerende kimeweka historia ya maendeleo baada ya kujenga shule mpya ya msingi ya kisasa, ikiwa ni sehemu ya matunda ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Viongozi wa kijiji hicho kilichopo kata ya Kemambo wilayani Tarime, wanasema shule hiyo itawezesha mamia wanafunzi kuanza kupata elimu ya msingi bila kutembea umbali mrefu.

“Utekelezaji wa mradi huu wa shule ya msingi mpya katika kijiji chetu umeenda vizuri. Ombi letu kwa serikali sasa ni kuifungua ili watoto wetu waanze kuitumia,” Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kerende, Marwa Gabogwe, aliwambia waandishi wa habari waliotembelea shule hiyo hivi karibuni.

Taarifa zinasema maandalizi ya kufungua shule hiyo yapo katika hatua za mwisho na wakati wowote itafungua milango kwa mamia ya wanafunzi ambao watahamishwa kutoka shule nyingine zilizopo katika kijiji hicho.

Kijiji cha Kerende kina vitongoji 10 ambapo wanafunzi kutoka vitongoji vitatu vya Mgosi, Isakahembe na Nyanyoka watakuwa wanufaika wa shule hiyo mpya.

Shule hiyo ya msingi ambayo itakuwa ya nne katika kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 8,000, imepewa jina la Mlima Mgosi ambao ni moja ya kivutio kiichopo kijijini hapo.

Shule nyingine za msingi za serikali zilizopo katika kijiji hicho ni Kerende, Ngeng’e na Ntimaro.

Shilingi zaidi ya milioni 300 zimetumika katika kutekeleza mradi huo ambao umehusisha ununuzi wa uwanja wa eneo la shule (ekari 10), ujenzi wa vyumba sita vya madarasa, ofisi ya walimu, vyoo vya walimu, wanafunzi na uwanja wa mpira.

Mojawapo ya vyoo vya shule hiyo

Utekelezaji wa mradi huo pia umejumuisha utengenezaji wa madawati ya wanafunzi 125 ambayo yapo tayari yakisubiri wanafunzi watakaofungua pazia katika shule hiyo.

Wakazi wa kijiji cha Kerende wanatoa shukrani kwa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa kutoa fedha ambazo zimefanikisha ujenzi wa shule hiyo kupitia mpango wake wa CSR.

Mgodi huo unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

“Mradi huu ulikuwa hitaji kubwa kwa sababu kijiji chetu kina vitongoji 10 na wanafunzi ni wengi. Hivyo, itakuwa na msaada mkubwa kwa watoto wetu,” anasema mkazi wa kijiji hicho, Mussa Magaigwa.

Pia, Magaigwa anaushukuru Mgodi wa North Mara kwa kuendelea kuchochea maendeleo ya kijamii katika vijiji vinavyouzunguka.

“Sisi tunaushukuru sana Mgodi wa Barrick North Mara kwa ajili ya miradi ya CSR inayotekelezwa kwenye vijiji vilivyo jirani. Hili ni jambo kubwa sana kwetu na tunashukuru sana,” anasema Magaigwa ambaye pia ni Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Kerende.

Naye Diwani wa Kata ya Kemambo, Rashid Bogomba, anasema ujenzi wa Shule ya Msingi Mgosi katika kijiji cha Kerende ni sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa miradi mipya inayofadhiliwa na Mgodi wa Barrick North Mara kupitia mpango wake wa CSR.

“Kazi inaendelea vizuri, fedha za CSR zimejenga shule mpya ya msingi Mgosi na majengo yote yamekamilika, haya ni maendeleo makubwa,” anasema Bogomba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) katika Mgodi wa Barrick North Mara.

Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa Mgodi wa North Mara umetumia shilingi bilioni 26.86 kugharimia utekelezaji wa miradi ya CSR 255 katika sekta za elimu, afya, barabara, maji, miradi ya kiuchumi na mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime tangu mwaka 2019 ulipokabidhiwa kwa Barrick.

Sekta ya elimu inatajwa kuchukua sehemu kubwa ya mabilioni hayo ya fedha za CSR yanayotolewa na Mgodi wa Barrick North Mara, ikifuatiwa na sekta za afya na maji.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages