NEWS

Monday, 9 November 2026

Iringa: Watu 21 wafariki katika ajali ya basi na roli, Rais samia atuma salamu za pole




Na Mwandishi Wetu
Iringa
------------

Watu 21 wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa katika ajali mbaya ya basi la abiria la Maokoto Bus Services na lori la mizigo katika eneo la njiapanda ya Kiponzero, Masumbo, kwenye barabara kuu ya Iringa-Mbeya.

Ajali hiyo ilitokea jana Jumatatu, saa moja asubuhi, wakati basi hilo lililokuwa likitoka kijiji cha Wasa, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, kuelekea Iringa Mjini lilipogongana na lori la mizigo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi, alisema watu 21 waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni wanaume 10, wanawake tisa na watoto wawili, wote miili yao ilipelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.

Majeruhi walipelekwa kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Hospitali Teule ya Ipamba na Zahanati ya Masumbo iliyopo Ifunda.

Kamanda Bukumbi alisema taarifa za awali za uchunguzi zinaeleza kuwa ajali hiyo huenda ilisababishwa na hitilafu katika mfumo wa breki za basi, hali iliyomfanya dereva kushindwa kulidhibiti kabla ya kugongana na lori hilo.

Hata hivyo, taarifa za Polisi zilieleza kuwa mazingira ya ajali hiyo yanaendelea kufanyiwa uchunguzi ili kubaini chanzo chake kwa uhakika.

Kufuatia ajali hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alituma salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, familia, ndugu, jamaa na Watanzania wote walioguswa na msiba huo..

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya ndugu zetu 21. Ninawaombea Mwenyezi Mungu awape wafiwa faraja, Subira na nguzu katika kipindi hiki kigumu, na awajalie uponyaji wa haraka wote waliojeruhiwa.

“Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema. Amina,” alisema Rais Samia.

Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa madereva kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, kuhakikisha vyombo vya moto vinakuwa katika hali nzuri na kuchukua tahadhari wanapokuwa barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo na majeraha.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages