
Wahitimu wa Darasa la Saba mwaka 2026 wakifurahia picha ya pamoja ndani ya mandari ya Muderspach Memorial Adventist School hivi karibuni.
Tarime
-------------
Shule ya Msingi Muderspach inayofahamika kama Muderspach Memorial Adventist School iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara, imeendelea kuthibitisha hadhi yake ya utoaji wa elimu bora, baada ya kufanya vizuri zaidi katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka 2026.
Matokeo hayo yameiwezesha shule hiyo yenye mchepuo wa Kiingereza kushika nafasi ya kwanza kiwilaya kati ya shule 45 zenye wanafunzi 40 na kuendelea.
Siri kubwa ya mafanikio hayo inatajwa kuwa ni nidhamu, usimamizi madhubuti wa kitaaluma, kujituma kwa walimu na ushirikiano wa karibu kati ya shule, wazazi na wadau wa elimu.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Mara Online News ofisini kwake leo Alhamisi, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Paul Basondole, amesema kati ya wanafunzi 83 waliofanya mtihani huo, 82 wamepata daraja A na mmoja daraja B.
Kwa mujibu wa Mwalimu Basondole, mafanikio hayo ni matokeo ya kumweka Mungu mbele katika kila jambo, kukamilisha mada zote za masomo kwa wakati na mazoezi ya kutosha ya mitihani kwa wanafunzi.
Amesema shule hiyo imekuwa na utaratibu wa kuhakikisha walimu wanakamilisha ufundishaji wa mada kwa wakati ili kuwapa wanafunzi nafasi ya kutosha ya kufanya marudio, kujisomea na kujipima kupitia mazoezi mbalimbali kabla ya mtihani.
Usimamizi wa walimu na nidhamu ya kitaaluma
Akifafanua kuhusu mikakati iliyotumika kuwaandaa wanafunzi, Basondole amesema shule imekuwa ikiwapa wanafunzi muda wa kutosha kujisomea chini ya usimamizi wa walimu, hatua iliyosaidia kuimarisha uelewa wao.
Amesisitiza kuwa usimamizi wa karibu wa wanafunzi, kujituma kwa walimu na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia ni miongoni mwa mambo yaliyochangia mafanikio hayo.
Matokeo ya Mtihani wa Darasa la Saba mwaka 2026 yanaonesha ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi waliopata ufaulu wa daraja A ikilinganishwa na mwaka 2025.
“Mwaka 2025, wanafunzi wetu 53 walipata daraja A na watano daraja B. Mwaka huu [2026], wanafunzi 82 wamepata daraja A na mmoja daraja B,” amesema Mwalimu Basondole.
Hali hiyo inaonesha ongezeko la wanafunzi 29 waliopata daraja A, yaani kutoka 53 mwaka 2025 hadi 82 mwaka 2026, huku idadi ya waliopata daraja B ikipungua kutoka watano hadi mmoja.

Mwalimu Mkuu wa Muderspach Memorial Adventist School, Paul Basondole, akiwa ofisini kwake.
Wazazi na walimu walivyochangia mafanikio
Wazazi wanatajwa kuchangia mafanikio hayo ya Shule ya Muderspach kutokana na ushirikiano wao mzuri na walimu, kutoa motisha na kuhakikisha ada za shule zinalipwa kwa wakati.
“Wazazi wamekuwa na mahusiano mazuri na walimu - wanatoa motisha kwa walimu na kulipa ada kwa wakati,” amesema.
Amesema ushirikiano huo umeiwezesha shule kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, huku walimu wakipata mazingira yanayowawezesha kujikita zaidi katika ufundishaji na malezi ya wanafunzi.
Akieleza kinachoitofautisha Muderspach na shule nyingine, Bosondole amesema imejikita katika kumweka Mungu mbele, kuimarisha juhudi za walimu na kusimamia maendeleo ya wanafunzi kwa karibu.
Ameongeza kuwa shule inatumia mbinu za ufundishaji wa vitendo na ziara za kielimu, ikiwemo ziara ya mafunzo ya wanafunzi katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na ya watumishi katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo.
Mbali na ubora wa ufundishaji, amesema shule imewekeza katika huduma na miundombinu bora inayomwezesha mwanafunzi kujifunza katika mazingira salama na rafiki.
Miundombinu na huduma hizo ni pamoja na zahanati ya huduma za afya shuleni, maji safi na salama, lishe bora, matumizi ya gesi safi ya kupikia, maabara ya kompyuta, lugha ya Kichina, usafiri wa uhakika kwa wanafunzi wa kutwa na vifaa vya kutosha vya kufundishia na kujifunzia.
Mikakati ya kudumisha ubora
Katika kuhakikisha mafanikio hayo yanakuwa endelevu, uongozi wa shule ya Muderspach umeweka mikakati ya kuboresha mazingira ya kazi na maisha ya walimu ili kuongeza ari na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mikakati hiyo inahusisha kulipa mishahara kwa wakati, kuhakikisha walimu wanaishi katika mazingira mazuri na kutoa motisha kwa walimu, watumishi wasio walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani na nidhamu.

Sehemu ya watumishi wa Muderspach Memorial Adventist School wakifurahia picha ya pamoja na mmoja wa wanafunzi wao.
Mwalimu Basondole amesisitiza kuwa shule inalenga si tu kudumisha kiwango cha cha ufaulu, bali pia kuendelea kukiboresha ili wanafunzi watakaofuata wanufaike na mazingira bora zaidi ya elimu.
Furaha ya matokeo bora ya kujivunia
Mwalimu Mkuu Basondole amesema watumishi na wadau wa Shule ya Muderspach wamepokea mafanikio hayo kwa furaha kubwa, akisema ni matokeo ya kazi iliyofanywa kwa bidii na mshikamano.
“Kweli tumefurahi sana sisi kama watumishi, wazazi, wadau mbalimbali wa shule, wakiwemo viongozi wetu wa Kanisa pamoja na wanafunzi wetu kuona kazi tuliyofanya kwa bidii imezaa matunda mazuri.
“Ushirikiano wa walimu, wazazi, wadau mbalimbali wa shule, viongozi wa Kanisa na wanafunzi ndiyo matokeo ya mafanikio haya ya kujivunia,” amesema Mwalimu Basondole.
Ujumbe kwa wazazi na jamii
Akitoa ujumbe kwa wazazi na walezi, Mwalimu Mkuu amewataka kuendelea kuiamini Muderspach, akisema ni miongoni mwa shule zinazojitahidi kutoa elimu ya kumjua Mungu sambamba na maarifa ya dunia kwa viwango vya juu.
“Wazazi watuamini kwani Muderspach ni miongoni mwa shule chache zinazofundisha maarifa ya kumjua Mungu na elimu dunia kwa viwango vya juu.,” amesisitiza Basondole.
Aidha, amewahakikishia wazazi kuwa shule itaendelea kuimarisha mazingira ya ufundishaji, malezi na ujifunzaji ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu inayowaandaa kukabiliana na changamoto za maisha.
Wito kwa wahitimu wa Shule ya Muderspach
Katika ujumbe wake kwa wanafunzi waliohitimu darasa la saba, Mwalimu Basondole amewataka kutoyachukulia mafanikio hayo kuwa mwisho wa safari yao ya elimu, bali kama mwanzo wa safari mpya yenye majukumu na fursa kubwa zaidi.
Amewataka kuendelea kuwa na nidhamu, bidii, kumcha Mungu na kujituma katika hatua zinazofuata za masomo yao, huku wakiendelea kuwa mabalozi wazuri wa Shule ya Muderspach katika maeneo watakayokwenda.
Muderspach memorial Adventist School ni Shule ya Kutwa na Bweni inayomilikiwa na kuendeshwa na kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo Dogo la North Mara Field.
No comments:
Post a Comment