
Muonekano wa sehemu ya majengo ya Shule ya Awali na Msingi Odikwa
Rorya
-----------
Shule ya Awali na Msingi Odikwa iliyopo wilaya ya Rorya mkoani Mara imeendelea kung’ara kitaaluma, baada ya kupata matokeo bora katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka 2026, ambayo yameiwezesha kushika nafasi ya kwanza kiwilaya.
Matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) Novemba 3, 2026, yanaonesha kuwa kati ya wanafunzi 34 wa shule hiyo waliofanya mtihani huo, 32 (wasichana 21 na wavulana 11) wamepata daraja A na wawili (msichana na mvulana) wamepata B.
Mafanikio hayo yanatajwa kuwa ni matokeo ya mfumo mzuri wa usimamizi, nidhamu ya kitaaluma, ushirikiano wa wadau wa elimu na mikakati ya kujenga utamaduni wa kufanya vizuri kwa wanafunzi na walimu.
“Siri kubwa ya mafanikio haya ya Shule yetu ya Awali na Msingi Odikwa imejengwa katika misingi minne muhimu tuliyojiwekea,” amesema Mkurugenzi wa shule hiyo, Mwl. Jacob Nguka Ogola, katika mahojiano na Mara Online News leo Alhamisi.
Nguka ametaja misingi hiyo kuwa ni ushirikiano (teamwork), uwajibikaji (accountability), uadilifu (integrity) na utekelezaji wa sera ya matumizi ya lugha ya Kiingereza kwa wote (English Language Policy).
Amesema misingi hiyo ndiyo inayounda utamaduni wa shule katika kufundisha, kujifunza, kusimamia majukumu na kuhakikisha kila mdau anatimiza wajibu wake kwa lengo moja la kupata matokeo bora.
Miaka minne ya matokeo bora
Takwimu zinaonesha kuwa Shule ya Awali na Msingi Odikwa imeendelea kufanya vizuri katika mitihani ya taifa ya darasa la saba kwa miaka minne mfululizo (2023-2026).
Mwaka 2023, wanafunzi wake 10 walipata daraja A, mwaka 2024, wanafunzi 22 walipata A, mwaka 2025, wanafunzi 24 walipata A na mwaka 2026, shule hiyo imeandika rekodi mpya baada ya wanafunzi wake 32 kupata daraja A.
Mwenendo huo unaonesha ongezeko la wanafunzi 22 waliopata daraja A ndani ya kipindi cha miaka mitatu, sawa na ongezeko la asilimia 220 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Mkurugenzi Nguka amesema mwenendo huo unaipa shule hiyo sababu ya kuendelea kuamini katika mfumo wake wa ufundishaji na usimamizi, huku ikiwajibika kudumisha na kuimarisha zaidi kiwango cha ufaulu.

Mkurugenzi Jacob Nguka Ogola (kulia) na wengine wakifurahia jambo shuleni hapo hivi karibuni wakati wa Mahafali ya Darasa la Saba 2026.
Mikakati nyuma ya ushindi
Mkurugenzi Nguka amesema mafanikio hayo yamechangiwa na utekelezaji wa mikakati maalumu ya kuongeza uelewa, kuimarisha uwezo wa wanafunzi na kuwaandaa kisaikolojia na kitaaluma kukabiliana na ushindani wa mitihani ya kitaifa.
Amesema shule hiyo ilihakikisha mitaala inafundishwa na kukamilishwa kwa wakati ili kuwapa wanafunzi nafasi ya kutosha kupitia masomo na kujiandaa kikamilifu kabla ya mtihani wa taifa.
Aidha, wanafunzi walifanyiwa mitihani mingi ya majaribio ili kupima uelewa wao, kubaini maeneo yenye changamoto na kurekebisha palipohitajika.
Hatua nyingine ilikuwa kufanya mitihani ya pamoja na shule kubwa kutoka nje ya wilaya na mkoa, ili kuwajengea wanafunzi uzoefu wa ushindani mpana na kupima uwezo wao dhidi ya wenzao kutoka mazingira tofauti.
Katika kuimarisha ari ya walimu, Mkurugenzi Nguka amesema shule yake pia imeweka mfumo wa motisha unaohusisha malipo ya shilingi 15,000 kwa mwalimu kwa kila A iliyopatikana kwenye somo analofundisha.
Amesema mfumo huo ni sehemu ya jitihada za kutambua mchango wa walimu na kuwahamasisha kuongeza juhudi katika utekelezaji wa majukumu yao shuleni.
Ni mafanikio yaliyobebwa na wadau wote
Pamoja na mikakati ya kitaaluma, Mkurugenzi Nguka amesisitiza kuwa mafanikio ya shule hiyo hayawezi kutenganishwa na mchango wa wazazi na walezi, wanafunzi na walimu.
Amesema wazazi na walezi wameendelea kutekeleza muhimu la kuhakikisha watoto wao wanapata mahitaji yao ya msingi ili waweze kujifunza katika mazingira yanayowawezesha kufanya vizuri kitaaluma.
Kwa upande wa wanafunzi, amebainisha kuwa bidii katika masomo, nidhamu na kujituma ndivyo vimewawezesha kunufaika na juhudi zinazofanywa na walimu.
Amesema walimu nao wamejipanga kutoa elimu inayozingatia misingi ya mitaala, huku wakiwalea wanafunzi katika misingi ya maadili ya dini na mwenendo unaokubalika katika jamii.
Odikwa kuendeleza utamaduni wa A
Kuhusu mipango ya baadaye, Mkurugenzi Nguka amesema shule yake haitaki kuridhika na mafanikio iliyoyapata, bali imejipanga kuendelea kudumisha kiwango cha juu cha ufaulu kwa kuhakikisha daraja A linabaki kuwa utambulisho wake.
Amesema ahadi ya shule hiyo kwa wazazi na walezi ni kuendeleza utamaduni wa ubora wa kitaaluma. "Jadi yetu itabakia A, hiyo ndiyo ahadi yetu kwa wazazi na walezi," amesisitiza.

Sehemu ya matukio ya wahitimu wa darasa la saba 2026 na walimu wao wakati wa mahafali hayo katika Shule ya Awali na Msingi Odikwa hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment