NEWS

Tuesday, 3 November 2026

TANAPA yazindua mradi wa umeme kuboresha utalii Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla



Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Mwishawa (katikati), Mkuu wa TANAPA Kanda ya Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Godwell Meng'ataki (kulia) na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Moronda Moronda, wakifurahia uzinduzi wa mradi wa umeme hifadhini hapo Novemba 2, 2026.

Na Mwandishi Wetu
Tabora
--------------

Mradi kabambe wa umeme uliogharimu shilingi milioni 380.2 umezinduliwa katika Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla mkoani Tabora ili kuchochea utalii, uhifadhi, uwekezaji na maenndeleo ya jamii zinazoizunguka.

Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Mwishawa, alizindua mradi huo Novemba 2, 2026 ili kuboresha huduma za utalii, maisha ya wananchi wa kijiji jirani cha Unyumbu na wafanyakazi wa hifadhi hiyo ya Mto Ugalla.

"Mradi huu umelenga kuchochea utalii, kuwavuta wawekezaji na kusogeza nishati ya umeme kukidhi shughuli za uzalishaji," alisema Kamishna Mwishawa.

Mkuu wa TANAPA Kanda ya Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Godwell Meng'ataki, alisema upatikanaji wa umeme utafungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi.

Meng'ataki alisema hiyo ni hatua itakayosaidia kuimarisha na kukuza sekta ya utalii katika Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla.

Naye Mkuu wa hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Moronda Moronda, alishukuru hatua iliyochukuliwa na TANAPA kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi na kuongeza hamasa ya huduma kwa watalii.

Moronda alisema mradi huo ulihusisha uwekaji wa nguzo 96 za zege na transforma yenye uwezo wa KVA 100.

Uwekezaji katika miundombinu kama ya umeme ni azima ya taifa kuboresha sekta ya utalii na kuimarisha uhifadhi endelevu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages