NEWS

Sunday 3 May 2020

Tarime Vijijini waweka vigezo vya mbunge wanayemtaka 2020

WANANCHI katika jimbo la Tarime Vijijini mkoani Mara wameweka bayana sifa za mbunge wanayemhitaji kupitia Uchaguzi Mkuu nchini utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Wakizungumza na Mara Online News kwa nyakati tofauti jimboni humo hivi karibuni, wananchi wamesema wanahitaji mbunge atayewasaidia kutatua kero mbalimbali zinazowakabili na kuliweka jimbo hilo katika ramani ya maendeleo endelevu.

Diwani mstaafu wa kata ya Kemambo, Agustino Sasi, amesema anatamani kuona jimbo hilo likipata mbunge mpya mwenye utashi wa kulistawisha katika nyanja za kijamii na kiuchumi.

“Tunahitaji mbunge mpya mwneye uwezo wa kutatua matatizo yetu yaliyodumu kwa miaka mingi sasa. Mfano, kuna tathmini iliyofanyika mwaka 2012 hapa Nyamongo kwa watu wanaoishi jirani na mgodi wa North Mara, lakini mpaka leo hakuna kilichotekelezwa. Tunataka mbunge atakayetatua hili,” amesema Sasi maarufu kwa jina la Neto.

Ameongeza kuwa angependa kuona safari hii anapatikana mbunge atayeunganisha wakazi wa jimbo hilo na kuondoa mgawanyiko wa kikoo.

“Wabunge waliopita wameshindwa kutetea hata mafao ya wazee wastaafu waboreshwe, wengi tunalipwa kidogo sana na wengine hawalipwi kabisa.

“Ndio maana safari hii tunataka mbunge anayefahamu matatizo ya wakazi wa jimbo la Tarime Vijijini na mwenye uwezo wa kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu,” amesisitiza Sasi.

Hata hivyo, Sasi ambaye ni mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema anaridhishwa na utendaji wa Rais Dkt John Magufuli akisema “Rais Magufuli anafanya kazi nzuri sana.”

Esther Masa kutoka kijiji cha Kegonga, amesema Tarime Vijijini inahitaji mbunge atakayejali na kutetea maslahi ya wanyonge.

“Tunataka mbunge atakayejali maisha ya watu wa chini, sio mbunge ambaye akichaguliwa anabadilisha namba za simu,” amesema Masa na kuongeza:

 Watalii wakitazama nyumbu wakivuka Mto Mara eneo la Kogatende 
“Lakini kingine kikubwa kwa wale ambao tunaishi jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti tunataka mbunge atakayesimama imara katika kutetea haki zetu.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti mstaafu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Amos Sagara, amesema jimbo hilo linahitaji mbunge mwenye mtazamo mkubwa wa kimaendeleo bila kujali chama cha siasa anachotaka.

Tarime inaongoza kuzalisha ndizi na kahawa aina ya Arabica Mkoani Mara 
“Mimi nashauri Tarime Vijijini tupate mbunge mwenye mahusioano ya kimaendeleo. Msingi uwe ni maendeleo, yaani mwenye kuthubuti bila kubagua vyama,” amesema Sagara ambaye pia ni Diwani mstaafu wa Kata ya Sirari.


Kutoka kata ya Muriba, Washington Matiko amesema jimbo hilo linahitaji mbunge mzelendo wa kweli na anayeshughulikia maendeleo ya wananchi kwa misingi ya usawa.

“Mbunge tunayemhitaji awe ni ambaye pia ataona matatizo ya wakazi wa Tarime Vijijini kama ni yake. Hatutaki mtu ambaye anatafuta ubunge kisha anatoweka jimboni,” amesema Matiko.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wanaomaliza kipindi chao mwaka huu wakiwa kwenye kikao
Diwani wa Viti Maalumu (CCM), Mariam Mkono, amesema shauku yake ni kuona jimbo hilo linampata mbunge atakayesimamia rasilimali zilizopo kwa ajili ya kubadilisha maisha ya wananchi.

“Tarime Vijiji tuna rasmili nyingi kama ikiwemo mgodi wa dhahabu na mbuga ya Serengeti, lakini bado hata miondombinu yetu sio mizuri. Kuna tathmini imefanyika pale Nyamongo lakini  wananchi hawajalipwa. Tunataka mbunge anayefahamu matatizo yetu.

“Lakini pia tunataka mbunge atakayeunganisha wananchi kuwa kitu kimoja na kutatua migogoro ya kikoo,” amesisitiza Mkono.


Wananchi wa Tarime wakiwa katika mkutano uliofanyika   jirani na mgodi wa North Mara kuzungumzia fidia 
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kerende, Muniko Magabe, amesema “Tunataka mbunge ambaye atakuwa karibu na wananchi, sio mbunge wa kutengeneza migogoro katika jamii.”

Magabe ameongeza “Kuna watu ambao sio wabunge lakini wanasaidia kutatua matatizo ya wananchi. Watu kama hao wakipata ubunge wanaweza kupeleka maendeleo yetu mbali.”

Uchunguzi uliofanywa na Mara Online News umebaini kuwa hadi sasa idadi ya wanasiasa wanaomezea mate jimbo la Tarime Vijijini mwaka huu ni zaidi ya 20, huku wanaowania jimbo la Tarime Mjini wakiwa zaidi ya 10.

Mbunge wa Tarime Vijijini anayemaliza muda wake ni John Heche (Chadema).

(Habari na Mwandishi Wetu, Tarime)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages