NEWS

Sunday, 28 July 2024

Nyambari Nyangwine alivyoitangaza Tanzania nchini India



Nyambari Nyangwine (mwenye kofia) akimkabidhi Waziri wa Utalii wa India, Shri Gajendra Singh Shekhawat zawadi ya bidhaa mbalimbali za Tanzania, Jijini New Delhi, India wiki iliyopita.
------------------------------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU
-----------------------------------------

Mfanyabiashara, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini, Nyambari Nyangwine amepata nafasi ya kukutana na Waziri wa Utalii wa India, Shri Gajendra Singh Shekhawat akiwa katika ziara ya kibiashara ambayo amesema imekuwa ya mafanikio makubwa.

“Pamoja na mambo mengine nilipata bahati ya kukutana na Waziri wa utalii wa India na kumpatia zawadi mbalimbali kutoka nchi yetu ya Tanzania,” Nyangwine ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime kupitia chama tawala - CCM, aliliambia gazeti hili mara baada ya kukutana na waziri huyo wa India, wiki iliyopita.

Baadhi ya bidhaa ambazo Nyambari alimzawadia waziri huyo wa India, ni kahawa, korosho na majarida mbalimbali yanayoonesha vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania.

Waziri huyo wa wa Utalii wa India alimshukuru Nyambari kwa zawadi hizo na kuahidi kushiriki katika hafla ya uzinduzi wa taasisi ya Nyambari Nyangwine Foundation ambayo inatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, Septemba mwaka huu.

Katika ziara hiyo, Nyambari pia alikutana na baadhi ya wafanyabiashara maarufu wa nchini India na kufanya nao mazungumzo Jijini New Delhi.

“Katika mazungumzo yangu na wafanyabiashara wa India wamekubali kushirikiana nasi kwenye uwekezaji wa shule, hospitali, elimu, kilimo, afya, madini, sayansi, teknolojia na mawasiliano, madini na viwanda mbalimbali vikiwemo vya kuongeza thamani ya mazao” alisema Nyambari.


Nyambari ambaye amefanya biashara ya uchapishaji yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 48 na nchi ya India tangu mwaka 2017 hadi sasa, alikuwa katika ziara ya kiabiashara ya wiki moja katika taifa hilo la barani Asia.

Alisema amefurahishwa na hatua ya wafanyabiashara hao wa India ya kumkubalia kushirkina nao kuwekeza nchini Tanzania, jambo ambalo litaunga mkono juhudu za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kukuza uwekezaji hapa nchini.

Nyambari pia alipata fursa ya kutembelea kituo kikubwa na maarufu cha television (runinga) nchini India, ambacho kinafahamika kama ZEE TV na kufanya nao mazunguzo ambayo alisema yatakuwa na matokeo chanya.

“Zee TV ni kituo cha television maarufu hapa India na nimekutana na mkurugenzi na menejimeti yake,” Nyambari alisema katika mazungumzo na Sauti ya Mara akiwa India.

Nyambari na ujumbe wake walipata pia fursa ya kutembelea viwanda mbalimbali katika miji ya New Delhi, Mumbai, Gujarat na Kolkata.

Baadhi ya viwanda hivyo ni vya uchapaji vitabu, katarasi, nguo na cha kuchakata korosho.

Nyambari pia alitembelea ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini India katika Jiji la New Delhi.

Aidha, Nyambari alikutana na kusalimiana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanazania, Dkt Tulia Ackson Jijini New Delhi.

Tayari Nyambari na ujumbe wake amerejea nchini Tanzania.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi
Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages