
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Eliakimu Mnzava akihoji uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
----------------------------------------------------
---------------------------------
Kwa mara nyingine, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara imeingia matatani kwa kupuuza maelekezo ya Rais kuhusu upulizaji wa dawa za kuua mbu.
Hayo yalibainika wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika halmashauri hiyo Ijumaa iliyopita.
Hali hiyo ilimshangaza na kumkasirisha Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Eliakimu Mnzava na kumsababisha kuuhoji zaidi uongozi wa halmashauri hiyo.
“Yaani Mheshimiwa Rais ameelekeza mpulize dawa za viuadudu kwa ku- combat (kukabili) malaria nyie hampulizi, hamkutenga fedha.
“Mnashindwa kutenga shilingi milioni tano na laki tano Serengeti wakati nimeambiwa hapa mnakusanya 3.8 bilioni na sasa hivi mnaenda kwenye 4 bilioni?
“Mnashindwa kutekeleza agizo la Kiongozi Mkuu wa Nchi, na ndio maana hapa malaria iko asilimia 23. Sasa nyie mko busy na nini katika hii Halmashauri kama hata kutekeleza maelekezo ya Kiongozi Mkuu wa Nchi hamtaki kufanya?
“Miradi ya maendeleo yote KfW (Benki ya Maendeleo ya Ujerumani), hakuna mradi wa maendeleo hata mmoja wa halmashauri hapa, ni milioni saba tu kikundi cha vijana bodaboda basi. Kwenye Mwenge wa Uhuru hakuna mradi wa halmashauri hata mmoja,” Mnzava alihoji.
Awali, uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ulimweleza Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kuwa mara ya mwisho kupuliza dawa ya kuua mbu ilikuwa mwaka 2022, na kwamba mwaka 2023 na 2024 hawakutenga fedha za shughuli hiyo.
Ni tatizo la kujirudia
Hiyo ni mara ya pili kwa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuingia matatani, kwani mwaka 2022 ilitajwa kuwa miongoni mwa halmashauri 43 nchini, zilizobainika kuwa na miradi ya umma yenye dosari mbalimbali.
Halmashauri hizo zilitajwa kwenye taarifa ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2022, iliyosomwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na wenye Ulemavu), Prof Joyce Ndalichako, mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, miradi 65 yenye thamani ya Sh bilioni 12.8 katika halmashauri 43 ilibainika kuwa na dosari, ikiwemo ujenzi chini ya kiwango, rushwa, uzembe, ubadhirifu na ukiukwaji wa mikataba, hivyo kusababisha miradi husika kutoakisi thamani ya fedha (value for money).
Kutokana na hali hiyo, Rais Samia aliziagiza mamlaka husika, zikiwemo TAKUKURU na ZAECA kuchunguza na kuchukua hatua stahiki didhi ya wote waliohusika katika ubadhirifu wa kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya umma.
Rais Samia alieleza kukerwa na viongozi walioshindwa kutekeleza majukumu yao, hadi mbio za Mwenge wa Uhuru zinapita na kubaini dosari za miradi ya kijamii katika maeneo yao ya kazi.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment