Viongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 wakikagua mradi wa maji uliotekelezwa na RUWASA katika kata ya Issenye wilayani Serengeti.
-------------------------------------------------
NA GODFREY MARWA, Serengeti
-----------------------------------------------
Wananchi takriban 10,000 katika vijiji vya Nyiberekera na Nyamisingi vilivyopo kata ya Issenye katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wameanza kunufaika na mradi wa maji ya bomba uliotekelezwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Hayo yalielezwa na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Serengeti, Mhandisi Deus Mchele wakati akisoma taarifa ya mradi huo wa maji kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Eliakimu Mnzava alipokwenda kufungua rasmi matumizi ya mradi huo, Ijumaa iliyopita.
Mhandisi Mchele alisema mradi huo umekamilika kwa asilimia 100, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba mbili kwa ajili ya mitambo ya maji, akibainisha kuwa utekelezaji wote umegharimu shilingi bilioni 1.955, kati ya hizo, wananchi walichangia shilingi milioni 15.4 pamoja na kutoa ardhi bure kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.
“Kukamilika kwa mradi huu kumeboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kutoka asilimia 18 hadi asilimia 100 ya watu wote 9,814 wa vijiji vya Nyiberekera na Nyamisingi katani Issenye,” alisema Mhandisi Mchele.
Akizungumza mara baada ya kufungua mradi huo, Mnzava alipongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwaboreshea Watanzania huduma ya maji.
“Mama [akimaanisha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan] hahesabu fedha anazoleta kwenye miradi ya maendeleo, anahesabu idadi ya miradi anayoleta kwa wananchi, ikiwemo inayolenga kumtua mama ndoo ya maji kichwani,” alisema Mnzava.
Aidha, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa aliwahimiza wananchi kukazania uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji kwa manufaa ya jamii nzima.
“Vyanzo vya maji viendelee kulindwa ili kuhudumia wananchi, Jumuiya za Watumia Maji zisimamie haki, kila mmoja apate maji kama Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alivyokusudia,” alisisitiza Mnzava.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment