Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Daniel Fungo akizungumza wakati wa tamasha la michezo kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Iramba wilayani Tarime lililoandaliwa na kanisa hilo kwa kushirikiana na Right to Play hivi karibuni.
----------------------------------------------
------------------------------------
Jamii imehamasishwa kuepuka vitendo vinavyoashiria ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya watoto wenye ulemavu kwani vinawakosesha amani na kuwafanya wasiishi kwa furaha kama ilivyo kwa wasio na ulemavu.
"Tuwe sababu ya watu wengine kuwa na furaha, kwa hiyo tusifanye mambo yatakayowafanya wenzetu wenye ulemavu wahisi wananyanyasika katika jamii.
“Hivyo kama ni elimu basi nao [wenye ulemavu] wapate kama watoto wengine kwa kuwa mpango wa Mungu ni sote tuwe na furaha,” alisema Joel Nkelebe kutoka Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe.
Nkelebe alikuwa akizungumza wakati wa tamasha la michezo lililoandaliwa kanisa hilo la AICT kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Right to Play katika viwanja vya Shule ya Msingi Iramba ya wilayani Tarime, Mara hivi karibuni.
Washindi wa michezo wakikabidhiwa zawadi wakati wa tamasha hilo.
-----------------------------------------------
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Gichogo Robert Mtundi alizishukuru taasisi hizo kwa juhudi kubwa zinazoonesha katika kupigania haki mbalimbali za watoto, ikiwemo kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata haki ya kupata elimu.
“Ninawashukuru sana AICT na Right to Play kwa kutuletea haya matamasha kwani wanaonesha jinsi walivyoweka juhudi kubwa katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi, lakini pia jamii inahamasishwa kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu na kutowaficha,” alisema Mwalimu Gichogo.
Kwa mujibu wa Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Daniel Fungo, lengo kubwa la taasisi hizo ni kuelimisha jamii umuhimu wa kuwapa watoto haki sawa, ikiwemo ya kupata elimu na kuwasaidia wenye changamoto za kiafya waweze kwenda shule.
Sambamba na hayo, AICT na Right to Play wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike na kuwajengea walimu na wanafunzi uwezo wa kupambana na changamoto mbalimbali kupitia matamasha ya michezo.
No comments:
Post a Comment