Wafanyakazi wa Migodi ya Dhahabu ya Barrick North Mara na Bulyanhulu wakifurahia picha ya pamoja baada ya kumaliza mbio za kilomita 12 katika eneo la Fort Ikoma wilayani Serengeti jana.
-------------------------------------------------
Mara Online News
-------------------------
Wafanyakazi 18 kutoka Migodi ya Dhahabu ya Barrick North Mara na Bulyanhulu wameshiriki mbio za Serengeti Anti-Poaching Run 2024 katika eneo la Fort Ikoma wilayani Serengeti.
Mbio hizo za kilomita 12 na tano, zilifanyika katika eneo la Fort Ikoma jana, ambapo zilishirikisha mamia ya wakimbiaji, wengi wao wakiwa vijana wa kiume na kike kutoka mikoa na taasisi mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.
Wakizungumza na Sauti ya Mara muda mfupi baada ya kumaliza mbio hizo, wakimbiaji hao walisema hiyo ni sehemu ya programu ya migodi ya Barrick inayojulikana kama In Reach Program inayowezesha wafanyakazi wake kuungana na jamii katika michezo mbalimbali.
“Lengo la programu hii ni kuhakikisha wafanyakazi wanashiriki michezo mbalimbali ili kujenga afya na ukakamavu wa miili.
“Mbio za leo [jana] zilikuwa nzuri na tumezifurahia sana,” alisema mkimbiaji Shida Kasanga ambaye ni Katibu Msaidizi wa In Reach program wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.
Mkimbiaji mwingine kutoka Barrick North Mara, Maugira Maugira alisema mashindano ya mbio ni sehemu ya michezo na mazoezi ambayo husaidia kujenga afya ya mwili na kuwaepushia watu magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari na moyo.
“Lakini pia michezo na mashindano kama haya ni sehemu ya kutukutanisha na jamii zinazozunguka migodi yetu na kuimarisha mahusiano.
“Kimsingi mbio za leo [jana] zilikuwa nzuri, tumekimbia huku tukifurahia kuona wanyamapori mbalimbali wakiwemo twiga, swala, nyumbu na pundamilia,” alisema Maugira.
Naye Michael Shoo kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu alisema: “Napenda mazoezi kama haya ya kukimbia kwa sababu yanajenga na kuimarisha afya ya mwili na akili.”
Mmoja wa wakimbiaji kutoka Migodi ya Dhahabu ya Barrick North Mara na Bulyanhulu akifurahia kumaliza mbio za kilomita 12 katika eneo la Fort Ikoma jana.
--------------------------------------------------
Akizungumza baada ya kuungana na wengine katika mbio hizo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marko aliwapongeza waandaaji na washiriki na kuwaomba kuendeleza utamaduni huo.
Mbio hizo za Serengeti Anti-Poaching Run zilitanguliwa na mbio za Serengeti Migration Marathon zilizofanyika juzi mjini Mugumu katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Mratibu wa Mbio za Serengeti Migration Marathon & Anti-Poaching Run, Mwalimu Samwel Mwita Nyankogoti alisema mashindano hayo yalianzishwa mwaka 2020 kutokana na wazo lililobuniwa na vijana wazawa wa wilayani Serengeti.
“Mbio hizi hufanyika kila mwaka kwa siku mbili mfululizo katika maeneo ya mjini Mugumu na Fort Ikoma, zikiratibiwa na Taasisi ya Michezo ya SETSA.
“Lengo kuu la mbio hizi ni kuhamasisha uhifadhi na ulinzi wa ikolojia ya Serengeti pamoja na kutangaza utalii wa ndani na nje ya nchi yetu, hasa magharibi mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti,” alisema Mwalimu Nyankogoti.
No comments:
Post a Comment