Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Eliakimu Mnzava akisalimiana na Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo wakati mbio hizo zilipokuwa jimboni humo wiki iliyopita.
-------------------------------------------------
--------------------------
Jitihada kubwa zimefanyika katika Jimbo la Musoma Vijijini za kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii ili kuboresha maisha ya wananchi katika jimbo hilo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru mwishoni mwa wki iliyopita.
Jimbo la Musoma Vijijini, linaloongozwa na Mbunge Prof Sospeter Muhongo, limejizolea sifa kwa utekelezaji makini wa miradi ya maendeleo ili kuwafanya wananchi kufaidi matunda ya uhuru.
Katika jimbo hilo Mwenge, ambao ulipokelewa kwa shangwe na maelfu ya wananchi, ulikagua na kuridhika na utekelezaji wa miradi saba ya kijamii yenye thamnani ya shilingi bilioni 3.5.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa shule (miradi miwili), zahanati, barabara, usambazaji wa maji kutoka Ziwa Victoria (miradi miwili) na kikundi cha vijana cha uchumi.
Akiwaongoza wananchi kuupokea Mwenge, Prof Muhongo alionyesha furaha isiyo kifani wakati akimkaribisha Kiongozi wa Mbio za Mwenge mwaka huu, Godfrey Mnzava.
Wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini waliishukuru serikali kwa utekelezaji wa miradi hiyo ambayo itasaidia kuboresha maisha yao.
Mwenge wa Uhuru ulikimbizwa mkoani Mara kwa siku tisa ambapo miradi 72 yenye thamani ya shilingi bilioni 25 ilikaguliwa ama kuzinduliwa katika sekta mbalimbali za kijamii.
No comments:
Post a Comment