Katibu Tarafa ya Inchage, Arif Abbas Rehan akipokea zawadi kutoka kwa Afisa Elimu ya Watu Wazima Halmashauri ya Mji wa Tarime, Tabu Lazaro katika hafla ya kufunga Juma la Elimu jana.
------------------------------------------
Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara imehitimisha maadhimisho ya Juma la Elimu ya kutathmini na kuhamasisha jamii kuhusu umhimu wa elimu kupitia vikundi na taasisi mbalimbali.
Maadhimisho hayo ambayo yalihitimishwa jana Ijumaa katika viwanja vya Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko, yalifanyika sambamba na maonesho ya biashara za wajasiriamali wadogo.
Baadhi ya washiriki hao ni KUBATA SACCOS, Menonite Compassion, Mogabiri Farm, Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime, Sent Collins Open School, Chuo cha Ualimu Tarime, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) na TK Movement.
Pia kupitia maadhimisho hayo ya Juma la Elimu, wanafunzi walionesha vipaji vyao katika michezo mbalimbali, ikiwemo ya kukimbia kwenye magunia, kutembea na maji kwenye chupa kichwani na kubeba yai kwa kijiko kwa kutumia mdomo.
Maadhimisho hayo yamelenga kutathmini masuala ya elimu ya watu wazima na elimu jumuishi, ikiwa ni pamoja na Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA), Mpango wa Elimu ya Sekondari kwa Waliokosa (MESKWA), Elimu Maalumu na Mpango wa Uwiano kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii, yakiwemo makundi yenye mahitaji maalum.
Mgeni rasmi katika hafla ya kuhitimisha maadhimisho hayo, Katibu Tarafa ya Inchage, Arif Abbas Rehan ambaye amemwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, amepongeza juhudi hizo na kusisitiza ulinzi wa watoto wa kike na haki yao ya kupata elimu.
"Niwapongeze kwa kazi nzuri na kubwa. Nipende kusisitiza kuwa walimu na wazazi tushirikiane kulinda Watoto wa kike na kufuatilia mienendo yao ili kuhakikisha wanasoma na kutimiza ndoto zao," amesema.
Awali, Afisa Elimu ya Watu Wazima katika halmashauri hiyo, Tabu Lazaro amesema matarajio ya maadhimisho ya Juma Elimu ni kuona kila mtoto anapata elimu, kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Lakini pia, matumizi sahihi ya zana za kufundishia na kujifunzia, kupinga ukatili dhidi ya wanafunzi na ndoa za utotoni, kupiga vita ngono zembe na uzingatiaji wa umuhimu wa chakula shuleni.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya Juma hilo la Elimu mwaka huu wa 2024 inasema: "Ujumuishi katika Elimu bila Ukomo kwa Ujuzi, Ustahimilivu, Amani na Maendeleo."
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Mkurugenzi Goldland Hotel ashiriki chakula cha pamoja na wanafunzi wa Moregas
>>Mahafali ya Darasa la 7 Odikwa 2024 yafana, CEO Mara Online aipa msaada wa kompyuta, printa
>>Mtandao wa X marufuku kutumika nchini Brazil
>> Gazeti la Sauti ya Mara latajwa Mkutano Mkuu wa HAIPPA PLC, CEO wake atunukiwa cheti cha pongezi
No comments:
Post a Comment