Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, Mohamed Sharif (mwenye suti ya bluu) katika picha ya pamoja na baadhi ya waandishi wa habari wa mkoani Mara baada ya semina iliyoandaliwa na TAKUKURU mjini Musoma jana kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kuelimisha wananchi kuepuka rushwa wakati wa uchaguzi. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara, Mugini Jacob, miongoni mwa washiriki wengine. (Picha na Mara Online News)
--------------------------------------------------
--------------------------------------
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara imekutana na waandishi wa habari wa mkoani humo kujadili namana bora ya kuendeleza elimu kwa jamii juu ya madhara ya rushwa katika uchaguzi wa viongozi.
Akizungumza katika semina ya siku moja iliyofanyika mjini Musoma jana, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, Mohamed Sharif alisema waandishi wa habari ni sehemu ya wadau muhimu katika vita ya kutokomeza rushwa.
Sharif aliwaomba waandishi wa habari kusaidia kuelimisha jamii iweze kuepuka vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi huo wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ujao.
Alitahadharisha kuwa vitendo vya rushwa katika uchaguzi vina madhara makubwa kwa maendeleo ya taifa, ikiwa ni pamoja na kuwa na viongozi ambao hawawezi kusimamia rasilimali za nchi ipasavyo.
“Tuna imani kwamba tukisimama pamoja na ninyi (waandishi wa habari) kwa sababu ya kuaminika kwenu tutafanikiwa zaidi,” alisema Sharif.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu wa Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC), Mugini Jacob aliishukuru TAKUKURU kwa kuandaa semina hiyo na kuahidi ushirikiano ambao utakuwa na matokeo chanya.
“Tunaahidi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika kuzuia na kupambana rushwa kupitia TAKUKURU, na kwa kufanya hivyo tataijenga Mara, tutajenga taifa letu,” alisema Jacob ambaye pia ni Mkurugenzi na Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Sauti ya Mara.
Takribani waandishi wa habari 15 kutoka vyombo mbalimbali walihudhuria semina hiyo ambayo iliandaliwa na ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Mara.
Semina hiyo imefanyika ikiwa ni miezi michache imebaki kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 15, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment