NEWS

Saturday, 3 August 2024

Wavuvi 100 Rorya wasalimisha zana haramu serikalini, wakabidhiwa halali



Ofisa Uvuvi Mkoa wa Mara, Ghati Kisyeri (kushoto) na Mtafiti kutoka TAFIRI, Dkt Benedicto Kashindye (katikati) wakimkabidhi Nyaki Warioba zana halali za uvuvi. Warioba ni miongoni mwa wavuvi 51 waliosalimisha zana haramu za uvuvi na kukabidhiwa na TAFIRI zana halali katika kijiji cha Kwibuse wilayani Rorya jana.
----------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Rorya
-------------------------------------

Wavuvi zaidi ya 100 waliokuwa wanajihusisha na uvuvi haramu katika Mto Mara wameripotiwa kusalimisha zana haramu zaidi ya 530 walizokuwa wakitumia kufanya uhalifu huo.

Zana hizo zimesalimishwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kupitia Mradi wa Usimamizi wa Ardhi Oevu katika bonde la Mto Mara unaotekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kwa kushirikiana na Shirika la WWF, halmashauri zinazozunguka mto huo na serikali ya mkoa, kwa ufadhili wa Shirika la Darwin Initiative la nchini Uingereza.

Akizungumza jana Agosti 2, 2024 kwenye hafla ya makabidhiano ya zana halali kwa wavuvi 51 waliosalimisha zana haramu 290 katika kijiji cha Kwibuse kilichopo wilaya ya Rorya mkoani Mara, Mtafiti kutoka TAFIRI, Dkt Benedicto Kashindye alisema katika kipindi hicho wametumia shilingi zaidi ya milioni 20 kununua zana za uvuvi kwa ajili wa wavuvi hao.

Dkt Kashindye alisema mradi huo wa miaka mitatu unatekelezwa kupitia elimu na hamasa kwa jamii ya wavuvi ambapo wamekuwa wakielezwa madhara ya matumizi ya zana haramu za uvuvi yanavyoathiri rasilimali za uvuvi katika bonde la Mto Mara.

Alisema baada ya kubaini kukithiri kwa uvuvi haramu kwenye mto huo - hali iliyokuwa ikitishia uhai wa baionuai, waliamua kutekeleza mradi huo baada ya kubaini kuwa matumizi ya nguvu ikiwemo kukamatwa kwa wavuvi na kuteketeza nyavu zao yalishindwa kuleta matokeo chanya kwa muda mfupi.

"Tunatoa elimu na kuhamasisha wote wenye zana haramu kuzisalimisha kwa hiari, kisha tunawapa zana halali, na katika kipindi cha miaka miwili yapo mabadiliko makubwa yametokea ingawa kuna upungufu wa bajeti ya kukidhi mahitaji ya wavuvi.

“Tunaendelea kutoa wito kwa serikali kutumia njia hii mbadala ili kutokomeza uvuvi haramu na kupunguza gharama za kufanya doria," alisema Dkt Kashindye.

Aliongeza kuwa kwa kipindi cha miaka miwili TAFIRI pia imekuwa ikifanya tafiti shirikishi zinazoshirikisha jamii katika kukusanya takwimu za uvuvi katika bonde la Mto Mara kwa lengo la kuishauri serikali kusimamia matumizi endelevu ya raslimali za uvuvi katika bonde hilo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zana hizo kwa baadhi wavuvi wa kijiji cha Kwibuse, Ofisa Uvuvi wa Mkoa wa Mara, Ghati Kisyeri aliwapongeza wavuvi walioamua kuachana na uvuvi haramu huku akitoa wito kwa wavuvi wote kuiga mfano huo.

Kuhusu vitendea kazi kwa ajili ya ulinzi, Ghati alisema mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wadau mbalimbali, wakiwemo TAFIRI watashirikiana kuona namna gani wanasaidia suala la vitendea kazi, ikiwa ni pamoja na boti kwa viongozi wa wavuvi katika ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi katika bonde la Mto Mara.

"Mkoa umeanzisha operesheni maalum kwa jina la Operesheni Fagia dhidi ya wavuvi wote wanaojihusisha na shughuli za uvuvi haramu na kwamba itakuwa endelevu na kutekelezwa chini ya usimamizi wa viongozi wa wavuvi, wavuvi wenyewe kwa kushirikiana na viongozi wa serikali pamoja na wataalamu wa sekta husika," alisema Ghati.

Aliwataka wavuvi na wananchi wote kuwa wasimamizi na walinzi wa rasilimali zilipo ndani ya mto huo ili uwe endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo, na kwamba mbali na kuwa chanzo cha maji, lakini pia mto huo ni chanzo cha uchumi kwa wakazi hao na mkoa wa Mara kwa ujumla.

Baadhi ya wavuvi wamesema bado wapo wavuvi wachache wanaoendeleza uvuvi haramu ndani ya Mto Mara huku wakiitaka serikali idhibiti upatikanaji wa zana haramu kwenye soko la Tanzania.

"Zana hizi haramu zimejaa huko mijini na ndio maana wavuvi wanazipata, serikali izuie wafanyabiashara kuingiza hizi zana kwenye soko, msako ufanyike kwa wenye maduka wanaouza ili wafilisiwe na kwenye mipaka yetu zana hizi zipigwe marufuku, hii itasaidia sana kutikomeza uvuvi haramu," alisema Petro Matiku.

Mwita Mtongori yeye aliiomba serikali kuangalia namna ya kuwawezesha zaidi ili waweze kufanya uvuvi salama kwa maelezo kuwa fedha walizokuwa nazo walitumia kununua zana haramu bila kujua madhara yake.

"Mmeona wenyewe hapa kuna wavuvi wamesalimisha nyavu zaidi ya mbili lakini kutokana na ufinyu wa bajeti wamepewa nyavu seti moja na kwa vile walitumia pesa nyingi kununua zana zisizofaa basi tunaomba serikali iweke mkono wake tuwezeshwe zaidi tuweze kumiliki nyavu zaidi ya moja kama ilivyokuwa awali," alisema Mtongori.
Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages